Share this Post

dailyvideo

MABALOZI WA NCHI ZA AFRIKA UMOJA WA MATAIFA WAMUAGA DK. MIGIRO



Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro ( mwenye kilemba) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mabalozi na Ma-naibu Balozi wanaoziwakilisha nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa, wakati wa hafla ya kumuaga iliyofanyika katika ukumbi wa Afrika House jijini New York. Naibu Katibu Mkuu anamaliza wafadhifa wake mwishoni mwa wezi huu.

Na Mwandishi Maalum.

Mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa, wamemuelezea Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha- Rozi Migiro, kama askari wa mwavuli aliyetua ardhini na mara moja akaanza kukimbia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa hafla waliyoandaa kumuaga Migiro, mabalozi hao wamesema mara tu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, hakubabaika, kwani alianza kazi mara moja kama wafanyavyo askari wa mwavuli.

Hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Mume wa Naibu Katibu Mkuu, Profesa Cleophas Migiro imefanyika siku ya jummane katika ukumbi wa mikutano wa Afrika House jijini New York.

Aidha mabalazi hao wameeleza kwamba, Naibu Katibu Mkuu, ameyatekeleza majukumu yake kwa uhodari wa hali ya juu, huku akiweka mbele maslahi ya Bara la Afrika.

“umetuwakilisha vema, umeibeba tochi ya afrika kwa uhodari ulikanyaga ardhi na kuanza kukimbia. Na hiki ni kielelezo cha cha wazi kwamba Tanzania chini ya Mwalimu Nyerere imewaanda vema wananchi wake kushika uongozi” akasema Balozi wa Ethiopia, Bw. Dawit Yohannes aliyezumgumza kwa niaba ya nchi za kanda ya Afrika ya mashariki.

Akasema kuwa Migiro anaondoka akiwa ameacha historia ya aina yake na kwamba mchango wake daima utaendelea kuenziwa katika Umoja wa Mataifa.

Naye Balozi wa Angola, Bw. Ismael Martins,akizungumza kwa niaba ya nchi za SADC yeyé amemuelezea Migiro kama mfano wa kiongozi bora aliyeonyesha utaamalu na uwezo wa hali ya juu katika utekelezaji wa majukumu yake. Na kwamba katika kuipindi cha uongozi wake yako mambo mengi ambayo ameyatekeleza kwa uhodari na uadilifu wa hali ya juu.

“kwa niaba ya nchi za SADC na kwa kuwa wewe unatoka katika SADC na SADC ilianzishwa Arusha nchini Tanzania, naomba nitoe shukrani zangi kwa niaba ya wezangu, tunakutakia kila lakheri huko uendeko na Mwenyezi Mungu akulinde” akasema Balozi wa Angola.

Akatumia fursa hiyo kumshukuru Professa Cleophas Migiro kwa namna alivyokubali mke wake na dada yao kutumia uzoefu na ujuzi wake kuitumikia jumuia ya Kimataifa.

“ Profesa, tunaomba tukushukuru, haikuwa rahisi kumuachia dada yetu kulibeba jukumu hili kubwa na lenye changamoto kubwa. Lakini kwa moyo mweupe ulijitolea na kumpatia ushirikiano wote. Nasiye tunakueleza kwamba tumemtunza vema dada yetu” akasema Balozi wa Angola.

Naye Balozi wa Gabon akizungumza kwa niaba ya nchi za Kanda ya Magharibi, Bw. Noel Nelson Messone, yeyé pamoja na kumshuru Profesa Migiro, amesema, Naibu Katibu Mkuu, ameipa heshima kubwa na ya aina yake Bara la Afrika ameonyesha kwa vitendo kwamba ameiweza kazi na ameonyesha utu na ubinadamu wa hali ya juu.

Naye mwenyekiti wa Kundi la Afrika kwa Mwezi wa June, Balozi wa Benin, Bw. Jean Francis Zinzou yeyé pamoja na mambo mengine amemuelezea Naibu Katibu Mkuu kama kiongozi mwanamke ambaye amekuwa mfano wa kuigwa na wanawake wengine hasa kutokana na ushupavu wake na uongozi ubora.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu amewashukuru mabalozi hao kwa ushirikiano mkubwa waliompatia katika kipindi chote cha miaka mitano na nusu ya uongozi wake.

Akimnukuu, Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini, Mzee Nelson Mandela. Migiro amesema “ kama nilikuwa nimesimama basi nilikuwa nimesimama juu ya mabega yenu ninawashukuru sana kwa kunipatia mabega yenu nikafika hapa nilipofika daima nitaienezi heshima hii”.

Akatumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viogonzi wote kwa kumpatia fursa hiyo athimu ya kuutumikia Umoja wa Mataifa.

Aidha Migiro pia akaishukuru familia yake akiwamo Mume wake, kwa ushirikiano, upendo, ushauri na uvumilivu wa hali ya juu mambo anayosema yamemuwezesha yeyé kutekeleza majukumu yake.

Akawataka mabalozi hao kuendeleza mshikamano wao, kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Mataifa na kuendelea kuisema Afrika na watu wake kila inapobidi.

“Bara letu bado linaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi, lakini ni bara linalopiga hatua kubwa kiuchumi na kimaendeleo. Ni bara ambalo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa analipa kipaubele cha aina yake. Kwa hiyo ninawaomba muendele kushirikiana na kusaidia na kuisaidia Afrika”. Akasisitiza.
Balozi wa Benin na mwenyekiti wa kundi la Afrika kwa mwezi wa Juni Bw. Jean Francis Zinsou akimkabidhi zawadi Naibu Katibu Mkuu, zawadi hiyo imetolewa na mabalozi wa Afrika.
Naibu Katibu Mkuu akiangalia zawadi aliyozawadiwa na Mabalozi.
Balozi wa Angola, Bw. Ismael Gasper Martins akizungumza kwa niaba ya nchi za SADC pamoja na mambo mengine amemshukuru Profesa Migiro kwa kumruhusu "dada yao" kuitumikia jumuia ya kimataifa, na kwamba wamemtunza vema dada yao ( Asha-Rose Migiro.
Balozi wa Gabon, Mhe Noel Nelson Messane akizungumza kwa niaba ya nchi za Kanda ya Magharibi.
Profesa Cleophas Migiro akifuatilia yale yaliyokuwa yakisemwa kuhusu Mke wake ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Asha- Rose Migiro
Balozi wa Ethiopia, Bw. Dawit Yohannes akizumgumza kwa niaba ya nchi za Kanda ya Afrika Mashariki, amemuelezea Migiro kama askari wa mwamvuli aliyetua ardhini na kuanza kazi mara moja.
Habari kwa hisani ya Michuzi Blog

Posted by Editor on 12:29. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for MABALOZI WA NCHI ZA AFRIKA UMOJA WA MATAIFA WAMUAGA DK. MIGIRO

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery