MAHAKAMA YA ICTR YAHAMISHA KESI YA LUTENI KANALI MUNYARUGARAMA
Na Ashura Mohamed, Arusha
Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda(ICTR) imekubali maombi ya mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo ya kuhamisha
kesi ya mtuhumiwa ambaye bado anasakwa na afisa wa zamani wa jeshi la
Rwanda,Luteni Kanali Pheneas Munyarugarama.
Hii
ni kesi ya nane na ya mwisho toka ICTR kuhamishiwa nchini Rwanda kwenda
kusikilizwa katika mahakama za nchi hiyo.
‘’Mahakama
inaamuru kesi hii kupelekwa katika mamlaka ya Jamhuri ya Rwanda ili mamlaka
hiyo iweze kupeleka kesi hiyo mara moja mbele ya Mahakama Kuu ya Rwanda kwa
ajili ya kusikilizwa kwa haraka,’’ sehemu ya uamuzi huo inasomeka.
Katika uamuzi wake, Mahakama iliyokuwa inaongozwa na Jaji Vagn
Joensen imemwamuru mwendesha mashitaka wa ICTR kumkabidhi Mwendesha Mashitaka
Mkuu wa Rwanda, nyaraka zote zinazounga mkono mashitaka dhidi ya mtuhumiwa
mapema iwazekanavyo.
Amri hiyo inatakiwa kutekelezwa katika kipindi kisichozidi siku
30 tangu kutolewa kwa amri ya mwisho ya kuhamishwa kwa kesi hiyo.
Mahakama ilielezea matumaini yake kwamba ‘’Jamhuri ya Rwanda,
kwa kukubali kesi toka ICTR, itatekeleza kwa vitendo ahadi iliyotoa juu ya
kuzishughulikia kesi hizo kwa nia njema, uwezo ilionao na utayari wa kuzingatia
viwango vya juu vya kimataiafa vya utendaji haki.’’
Luteni Kanali huyo anashitakiwa kwa makosa ya mauaji ya kimbari,
kula njama za kufanya mauaji hayo, uchochezi na uhalifu dhidi ya binadamu kwa
kuua, kuteketeza kizazi, ubakaji na utesaji.
Munyarugarama alikuwa Kamanda wa kambi ya jeshi ya Gako katika
wilaya ya Kanzenze,eneo la Bugesera, katika mkoa wa Kigali Vijijini kati
ya mapema 1993 na Mei 1994.
Alizaliwa Januari mosi, 1948 katika wilaya ya Kidaho mkoani
Ruhengeri, Kaskazini mwa Rwanda.
Kesi nyingine zilizohamishiwa tayari nchini Rwanda zinahusu
watuhumiwa wawili wa ICTR, mchungaji Jean Uwinkindi na kiongozi wa wanamgambo
wa Interahamwe Bernard Munyagishari, watuhumiwa watano ambao bado wanasakwa,
wakiwemo mameya watatu, Charles Sikubwabo, Ladislas Ntaganzwa na Aloys
Ndimbati, Inspekta wa zamani wa polisi, Fulgence Kayishema na meneja mmoja wa
mgahawa, Charles Ryandikayo.
Kwa Hisani ya Full Shangwe Blog
Kwa Hisani ya Full Shangwe Blog
Posted by Editor
on 19:04.
Filed under
eastafricannews,
feature
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0