Share this Post

dailyvideo

POSHO ZA MADIWANI ZAPANDAWAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema kuanzia mwaka huu madiwani wote nchini wataanza kulipwa viwango vipya vya posho vilivyoboreshwa.Akisoma hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), kwa mwaka 2012/13, Pinda alisema tangu mwaka jana Serikali iliahidi kuwaongezea posho madiwani.

“Wakati nahitimisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya ofisi yangu mwaka jana, niliahidi kuwa Serikali itaangalia upya viwango vya posho za madiwani kwa lengo la kuviongeza,” alisema Pinda na kuongeza;

“Sasa zoezi hilo limekamilika na kuanzia mwaka 2012/2013 madiwani watalipwa viwango vipya vya posho vilivyoboreshwa.”

Alisema ili kuwawezesha viongozi wa mikoa na wilaya kutekeleza majukumu yao , Serikali imetoa mafunzo kwa wakuu wa mikoa na wilaya na kutekeleza ahadi yake ya kutoa mafunzo kwa madiwani 4,451 nchini. 

“Ni imani yangu kwamba baada ya mafunzo hayo, utendaji kazi wa viongozi hao utakuwa ni wa ufanisi zaidi,” alieleza matarajio yake Pinda.

Mbali na kuongezwa kwa posho hizo, aliwaagiza wakurugenzi watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kubandika kwenye mbao za matangazo katika vituo vyote vya utoaji huduma, kiasi cha fedha kinachopokelewa kila mwezi na matumizi yake.

Kwa muda mrefu madiwani nchini wamekuwa wakilalamikia kiwango cha posho wanachopata sambamba na mishahara, huku wakishinikiza kulipwa kama wabunge.

Mbali na posho hizo, ameonya kwamba watumishi  wa Serikali watakaobainika kutafuna fedha za umma, watavuliwa madaraka na kufikishwa katika vyombo vya sheria, na hakuna atakayehamishiwa kituo kipya baada ya kuharibu kituo cha awali.

Alisema mwaka 2010/11, Serikali ilitangaza nia ya kuanzisha maeneo mapya ya utawala ya mikoa minne ya Simiyu, Katavi, Njombe na Geita pamoja na wilaya mpya 19 na Tarafa 34, lengo likiwa ni kusogeza na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Tayari Serikali imeyaanzisha rasmi maeneo hayo na uteuzi wa viongozi wa kusimamia mikoa na wilaya hizo umefanywa,” alisema Pinda. 

Kuhusu ripoti ya CAG
Akizungumzia viongozi watakaobainika kutafuna mali za umma ambao walitajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Pinda alisema watachunguzwa na wakibainika watavuliwa madaraka.

“Wakivuliwa madaraka waliyonayo watafikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema Pinda na kuongeza;
“Serikali haitawahamisha watumishi wa aina hiyo, bali hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi.”

 Pinda aliwataka watendaji wakuu wa Serikali, bodi za wakurugenzi wa mashirika ya umma na madiwani kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika kusimamia fedha za umma kwa mujibu wa sheria, taratibu, miongozo na kanuni zilizopo, na kubandika matumizi hayo kwenye mbao za matangazo.
Alisema hatua hiyo itawezesha wananchi kufuatilia matumizi ya fedha zilizopelekwa kwa ajili ya utoaji huduma kwenye maeneo yao.

Ununuzi wa magari
Akizungumzia ununuzi wa magari ya Serikali  maarufu kama mashangingi, Pinda alisema Serikali inaendelea kupunguza matumizi yasiyo na tija hasa ununuzi wa magari makubwa ya kifahari, ambayo gharama zake ni kubwa.

Alisema kwa kuanza,  magari yatakayonunuliwa yatakuwa ni yale yasiyozidi ukubwa wa injini wa CC 3,000 kwa viongozi na watendaji wakuu na yasiyozidi CC 2,000  kwa watumishi wengine ambao wanastahili kutumia magari ya Serikali.

Kambi ya Upinzani
Kwa upande wake Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amemlipua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kuzuia uchaguzi wa mitaa na vitongoji ili kupisha Chaguzi za CCM.

Mbali na hilo, ameitaka Serikali kutolea ufafanuzi suala la gharama zilizotumika katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania, kama kweli zilikuwa Sh64 bilioni.

Akisoma maoni yake kwa Ofisi hiyo ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2012/13,  Mbowe alisema kusimamishwa kwa baadhi ya chaguzi kumeidhinishwa na waziri mkuu kutokana na chombo kinachosimamia  kuwa chini yake. “Chombo cha kusimamia uchaguzi huo kipo chini ya Waziri Mkuu ambaye ndio amekuwa akitoa kauli ya kusimamisha ili kupisha uchaguzi wa CCM,” alisema Mbowe na kuongeza:

"Kambi ya Upinzani, tunamtaka Waziri Mkuu kuwaeleza wananchi kuwa anachukua hatua gani kwa hili ambalo limetokea kwani limesababisha baadhi ya mitaa na vitongoji kutokuwa na viongozi kwa sababu tu chama chake kinafanya chaguzi.”

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema Serikali imekuwa ikishindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na kutokuwa na fedha huku ikitumia fedha nyingi katika sherehe mbalimbali za kitaifa.

“Katika maadhimisho ya miaka 50 (ya uhuru) yaliyofanyika mwaka jana, gazeti la The Citizen linalochapishwa na Mwananchi Communications Limited lilisema kuwa Serikali ilitumia Sh64 bilioni na mpaka sasa haijakanusha taarifa hizo, kitendo kinachoashiria kuwa ni kweli,” alisema Mbowe na kuongeza:

"Serikali inatakiwa kulitolea ufafanuzi ili wananchi waweze kujua ni kiasi gani cha fedha kilichotumika kuliko kuendelea kubaki kimya na maswali mengi yakitanda.”
Mbowe alifafanua kuwa umefika wakati kwa Serikali kuchagua sherehe ambazo ni za muhimu na kuwa zinaadhimishwa, kuliko hivi sasa, ambapo imekuwa ikifanya hivyo kila sherehe na kuligharimu taifa.

Waliofukuzwa UDOM
Mbowe alikitaka Chuo Kikuu cha Dodoma kuwarejesha wanafunzi waliofukuzwa mwaka jana kutokana na kupinga kumaliza masomo bila kufanya mazoezi kwa vitendo.

 “Kuwanyima haki zao wanafunzi ni kuendelea kuliweka taifa katika hali mbaya na kinachotakiwa ni kuwarejesha masomoni mara moja, ili wamalize masomo yao kuliko kuwaacha wakiendelea kukaa nyumbani,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Vitisho na manyanyaso dhidi yao ni dhambi ambayo itawarudia siku moja, na kinachotakiwa ni kuwarudisha wanafunzi  wote haraka iwezekanavyo.”


Habari na - Florence majani kutoka Dodoma, Fidelis Butahe na Ibrahim Yamola, Dar

Posted by Editor on 12:29. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for POSHO ZA MADIWANI ZAPANDA

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery