Share this Post

dailyvideo

Jaji Mkuu kusikiliza rufaa ya Lema



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, atakuwa miongoni mwa jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani watakaosikiliza rufani ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.



Jaji Chande atashirikiana na majaji wengine wa mahakama hiyo, Natalia Kimaro na Salum Massati kusikiliza rufani hiyo namba 47/2012 ya mwaka 2012.

Orodha ya awali ilionyesha kuwa rufani hiyo ya Lema kupinga kutenguliwa kwa matokeo ya uchaguzi wa ubunge katika uchaguzi wa mwaka 2010, ingesikilizwa na Jaji Mbarouk Salim Mbarouk, Jaji Kimaro na Jaji Salum Massati.

Hata hivyo, ratiba mpya inaonyesha kuwa Jaji Mkuu Chande, amechukua nafasi ya Jaji Mbarouk.

NIPASHE imeshuhudia ratiba ya vikao vya mahakama hiyo iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Maxmillian Malewo, ambayo imebandikwa kwenye ubao wa matangazo.

Hata hivyo, haikufahamika ni sababu zipi zimesababishwa kuondolewa kwa Jaji Mbarouk katika orodha ya majaji wa kusikiliza rufani hiyo. Hakuna ofisa yeyote katika ofisi ya Msajili aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo.

Rufani hiyo inatarajiwa kusikilizwa Septemba 20, mwaka huu na baadaye kupangiwa siku ya kusomwa kwa hukumu.

Wakili wa Lema, Method Kimomogoro, alisema kuwa atashirikiana na Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu katika shauri hilo.

 Kimomogolo alisema badiliko hilo la kuongezeka Tundu Lissu, tayari ameshaitaarifu Mahakama tangu Agosti 28, mwaka huu.

Lema, aliandika madai 18 na kuyawasilisha Mahakama ya Rufaa baada ya kutenguliwa ubunge wake Aprili 5, mwaka huu.

Lema katika hoja zake, anaiomba Mahakama ya Rufaa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu uliomtengua ubunge wake.

Pia anaiomba Mahakama ya Rufaa kumtangaza kuwa mbunge halali wa Jimbo la Arusha Mjini pamoja na kuamuru walalamikiwa katika kesi hiyo walipe gharama za rufaa hiyo na kesi ya Mahakama Kuu.

Kadhalika, Lema anamlalamikia Jaji Gabriel Rwakibarila, wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, aliyesikiliza kesi hiyo kwamba hakutoa hukumu kwa kuzingatia ushahidi halisi uliotolewa mahakamani, bali alifanyia kazi uvumi.

Hoja nyingine ya Lema ni kwamba Jaji Rwakibarila alikosea kuamuru mpiga kura yeyote kuruhusiwa kupinga matokeo ya uchaguzi hata kama haki zake za msingi hazijaguswa.

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitengua ubunge wa Lema katika kesi ya kupinga matokeo yake iliyofunguliwa mahakamani hapo na walalamikaji hao ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Shauri lililopewa namba 13/2010, lilifunguliwa na walalamikaji hao wakipinga matokeo hayo na kudai kuwa Lema alikiuka kanuni, maadili, taratibu na sheria za uchaguzi na kesi hiyo kusikilizwa na Jaji Rwakibarila ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.

Jaji Rwakibarila aliteuliwa kusikiliza kesi hiyo iliyovuta watu wengi kufuatia Jaji Aloyce Mujulizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kujitoa, baada ya upande wa walalamikaji kumkataa kwa maelezo kuwa haukuwa na imani naye. 

Katika shauri hilo, walalamikaji walidai kuwa Lema wakati wa kampeni zake alitoa lugha za matusi, kashfa na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo kupitia CCM, Dk. Batilda Burian katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Katika hukumu yake, Jaji Rwakibarila alisema amebaini kuwa katika mikutano 60 ya kampeni za uchaguzi huo, mikutano minane iligundulika kuwa Lema alikiuka maadili ya kampeni za uchaguzi.

Jaji Rwakibarila alisema Mahakama imebatilisha matokeo ya ubunge wa Lema kutokana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.

Alisema madai hayo pamoja na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, Mahakama imeridhika kwa kuwa Lema alikiuka sheria na vifungu vyake vinavyokataza kufanya kampeni kwa misingi ya ubaguzi wa kidini, ujinsia na kikabila, hivyo kwa misingi hiyo Mahakama inatengua matokeo ya uchaguzi wa ubunge wake kama walivyokuwa wameomba walalamikaji.

Jaji huyo pia alimwamuru Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, George Hurbert, kupeleka nakala ya hukumu ya kesi hiyo katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa hatua inayofuata.

Lema alikuwa akitetewa na Method Kimomogoro wakati wadai wakiwakilishwa na mawakili wawili, Alute Mungwai na Modest Akida, huku upande wa serikali ukitetewa na Timon Vitalis na Juma Masanja.


HABARI NA CYNTHIA MWILOLEZI
CHANZO: NIPASHE

Posted by Editor on 11:31. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for Jaji Mkuu kusikiliza rufaa ya Lema

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery