Kilio cha wabunge chanasa watatu
Hatimaye kilio cha wabunge, Hamad Rashid Mohamed (Wawi - CUF), na Ezekiel Wenje (Nyamagana -Chadema) cha wageni kutorosha nje ya nchi dhahabu na kuikosesha serikali mabilioni ya shilingi kimezaa matunda baada ya raia watatu wa nje kukamatwa na polisi kwa tuhuma hizo.
Tuhuma hizo zilitolewa na Hamad Rashid na Wenje katika mkutano wa Bunge uliopita mjini Dodoma na kutaka serikali iwakamate watu hao ambao mmoja wao alikuwa anafanya mambo kama amenunua viongozi wa serikali. Wenje pia aliwasilisha vielelezo vya hujuma hizo kwa Spika.
Ikifanyia kazi tuhuma hizo, jana Naibu Waziri wa Nishati na Madini (anayeshuhulikia madini), Stephen Masele (pichani), alisema Jeshi la Polisi nchini linawashikilia raia watatu wa nje ambao viongozi kampuni ya uchimbaji wa dhahabu ya Aureus Limited, baada ya kubainika kuficha taarifa za mauzo ya madini hayo na hivyo kuikosesha serikali mapato yenye thamani ya Sh. bilioni 10.7.
Aidha, mmiliki wa kampuni hiyo ambaye ni raia wa Ubelgiji anaishi Barcelona nchini Hispania, Marc Rene Roelandts, anasakwa na serikali kwa tuhuma hizo kupitia Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) ili kumkamata na kumrejesha nchini ili ajibu mashtaka hayo.
Roelandts inasemekana kuwa anamiliki asilimia moja ya hisa moja na Kampuni ya MS Quaester Limited ya huko Mauritius inayomiliki hisa 999.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Masele alisema kuwa watu hao walikamatwa Jumatatu wiki hii mkoani Mwanza.
Masele alisema kampuni hiyo inamiliki mitambo miwili ya uchenjuaji iliyopo katika kijiji cha Nyarugusu wilayani Geita na mtambo wa pili upo Nyakato jijini Mwanza.
Aliwataja wanaoshikiliwa na polisi mkoani Mwanza kuwa ni raia wa Uholanzi ambaye ni kiongozi wa shughuli zote za kampuni hiyo, David Gommeren (43); raia Afrika Kusini ambaye ni Mkuu wa Uzalishaji wa kampuni hiyo, Gideon Ludwick na raia wa Israel, Andrey Vash (44).
Masele alisema Agosti hadi Septemba mwaka jana, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ulifanya ukaguzi wa hesabu za fedha wa kampuni hiyo ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Minextech (Kampuni ya uchenjuaji wa marudio ya dhahabu) kwa wachimbaji wadogo kwa kutumia Teknolojia ya Kemikali ya Sayanaidi.
“Ukaguzi huo uligundua kasoro kadhaa zilizoikosesha serikali mapato ikiwa ni pamoja na Kampuni ya Minextech kuficha taarifa zake za mauzo ya dhahabu kiasi cha kilo 63.27 yenye thamani ya Shilingi 2,763,426,787 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2010,” alisema naibu Waziri.
Kwa mujibu wa Masele, udanganyifu huo ulibainika baada ya kulinganisha na taarifa za mauzo ya dhahabu zilizowasilishwa serikalini na kampuni hiyo katika kipindi husika.
“Kampuni ya Minetech kutolipa kiasi cha Shilingi 9,085,031,656 kama VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) ya mauzo ya dhahabu katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2010,” alisema.
Alisema pia kampuni hiyo ilibainika kutolipa Sh. 252,683,678 kama kodi ya mishahara (PAYE) katika kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2010.
Naibu Waziri huyo alisema kuwa vile vile, kampuni hiyo ilibainika kutolipa mrabaha wa Sh. 371,026,716 katika kipindi cha kati ya mwaka 2006 hadi 2010.
Masele alisema hatua stahiki zinaendelea kuchukuliwa na serikali ili kuhakikisha malipo hayo yanafanyika.
“Serikali imechukua hatua za awali za kuhakikisha kuwa wahusika wote wanakamatwa na kufunguliwa mashitaka. Tayari viongozi wakuu wa kampuni hiyo wapo mikononi mwa Jeshi la Polisi na uchunguzi zaidi unaendelea kabla ya serikali kuchukua hatua zinazostahili,’ alisema na kuongeza:
“Tukio hili linadhihirisha wazi kuwa Kampuni ya Aureus Limited ilikuwa imekusudia kuficha kiasi halisi cha uzalishaji wake kwa lengo la kukwepa kulipa mrabaha na kodi stahiki.”
Alisema hatua za kisheria zitakazochukuliwa ni pamoja na kufutiwa leseni na kutaifishwa kwa mgodi ulioko Nyarugusu.
Serikali imejipanga vizuri kubaini na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaojihusisha na udanganyifu katika shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchni, kwa mujibu wa Masele.
“Wote watakaopatikana na kosa hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni zao na kuzuiliwa kujishughulisha na shughuli za madini hapa nchini,” alisema.
Kadhalika, Masele alisema wawekezaji hao walikuwa wakituhumiwa kuwadharau viongozi wa serikali, kutoa lugha za matusi na kejeli kwa nyakati tofauti, ikiwemo wakati wa ziara ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai Nahodha, ya kuutembelea mgodi huo wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Pia, wawekezaji hao wanadaiwa kwa makusudi kukiuka makubaliano kati yao na serikali yaliyofikiwa kwa lengo la kudhibiti shughuli zake za uzalishaji.
Masele alisema Septemba 9, mwaka huu, waliwadanganya wakaguzi kuwa wasingefanya uzalishaji wa dhahabu siku hiyo na badala yake wangefanya kesho yake Septemba 10.
Hata hivyo, alisema wakaguzi hao waligundua kuwa Septemba 10 kulifanyika uzalishaji, baada ya kuelezwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya wabunge kulalamikia kampuni hiyo kutorosha nje madini hayo.
Hamad Rashid aliwahi kulieleza Bunge kuwa kampuni hiyo imekuwa ikizalisha wastani wa kilo 15 kwa wiki na kuzitorosha nje ya nchi bila kuilipa kodi serikali.
Masele alisema kufuatia tuhuma hizo, Wizara kupitia TMAA ilichukua hatua za haraka kwa kuweka usimamizi makini wa shughuli za uzalishaji za kampuni hiyo ili kubaini ukweli.
HABARI NA SHARON SAUWA
CHANZO: NIPASHE




