Wanaharakati wataka sheria ya gesi, mafuta
(1).jpg)
Serikali imeaswa kufuta utoaji wa zabuni za uchimbaji wa mafuta na gesi iliyogundulika hivi karibuni hadi pale itakapokuwa imekamilisha taratibu za kuwa na sera na sheria zenye manufaa kwa ustawi wa Watanzania.
Wito huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na asasi tatu za kiraia za Sikika, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Hakielimu kwenye taarifa yao ya pamoja waliyoitoa mbele ya wahariri wa vyombo vya habari.
Akizungumza kwa niaba ya asasi hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria alisema ili maliasili hiyo iweze kutatua matatizo yanayowakabili wananchi kama yalivyoainishwa kwenye Ripoti ya Serikali ya Umaskini na Maendeleo ya Wananchi ya mwaka 2011, kuna umuhimu wa serikali kutokimbilia kwenye uchimbaji bila ya uwepo wa sera na sheria thabiti.
“Hivyo kuna umuhimu wa kuupitia upya mchakato mzima wa uchimbaji wa rasilimali hiyo kuanzia kwenye utoaji mikataba na leseni, shughuli za udhibiti na ufuatiliaji, makusanyo ya mapato na uwazi kwenye utekelezaji wa sera na miradi endelevu," alisema.
Kiria alisema ni muhimu serikali ikahakikisha kwamba kuna mashauriano ndani ya serikali yenyewe, Bunge, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kuepukana na sera dhaifu, ufisadi na uwezekano wa nchi kuingia katika machafuko kama inavyotokea katika nchi zingine, rasilimali hii ilipogundulika.
Alipendekeza kufanyiwa kazi kwa mambo matano kabla ya kuruhusiwa kwa uchimbaji wa rasilimali hiyo yanayojumuisha utoaji wa mikataba na leseni, shughuli za udhibiti na ufuatiliaji, ukusanyaji wa kodi na mirabaha, mgawanyo na matumizi ya mapato pamoja na utekelezaji wa sera endelevu na miradi.
Wito huu wa asasi hizi unakuja wakati ripoti ya serikali ikiwa imetangaza kusitisha zabuni iliyoitangaza kwa ajili ya utoaji wa leseni za uchimbaji wa mafuta na gesi iliyogundulika.
Aidha, unatolewa wakati ambapo ripoti ya serikali ya umaskini na maendeleo ya wananchi ya mwaka 2011, ikionyesha kuwa umaskini bado ni tatizo kubwa miongoni mwa wananchi na vita dhidi ya ufisadi ikiwa bado haijaleta mafanikio makubwa.
habari NA RAPHAEL KIBIRITI
CHANZO: NIPASHE




