TOP NEWS: WATANZANIA 120 WASHIKILIWA MAHABUSU ZA IRAN
Na Mwandishi wetu
Watanzania
takribani 120 wanashikiliwa katika mahabusu za Iran kwa makosa mbalimbali kwa
miaka minne sasa huku jitihada za serikali ya Tanzania kuwanusuru zikiwa
zimekwama.
Watanzania hao wanashikiliwa kwa makosa mbalimbali, yakiwamo ya kukamatwa na
dawa za kulevya na kuingia Iran bila vibali.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Christopher Mvula, alithibitisha kushikiriwa kwa
Watanzania hao katika mahabusu nchini Iran.
Mvula alisema mbali na Watanzania hao kushikiliwa, mazungumzo kati ya Tanzania
na Iran kuhusu kuwarejesha nchini yanaendelea, lakini suala hilo linakuwa gumu
kutokana na nchi hizo kutokuwa na sheria ya kubadilishana wafungwa.
Mvula aliongeza kuwa kikwazo kingine ni kutokana na Tanzania kutokuwa na
ubalozi nchini Iran badala yake na kutumia ubalozi wa Falme za Kiarabu.
Alisema Iran kuwaachia watu hao siyo kitu cha haraka na rahisi kutokana na
watuhumuiwa wengi kukamatwa na makosa makubwa.
Mvula alisema kuna makosa madogomadogo ambayo yanaweza kuzungumkika kama vile
ya kusingiziwa, kuiba, lakini siyo yale makubwa kama ya dawa za kulevya.
Alisema vijana wengi wa kitanzania waliokamatwa Iran wamekamatwa kwa tuhuma
za makosa hayo na wachache makosa madogo kama uzamiaji na ndiyo maana zoezi la
kuwaachia na kuja kutumikia adhabu nchini linachukua muda mrefu.
Mmoja wa ndugu wa Watanzania hao ambaye pia ni Mwenyekiti wa wazazi wa ndugu
hao, Bidie Bulushi, alisema lichas ya vijana wao kushikiliwa Iran kwa muda huo,
serikali haijaonyesha jitihada za kuwanusuru.
Alisema miongoni mwao ni mdogo wake wa tatu, Ali Seif, aliyeingia Iran mwaka
2005 kwa lengo la kutafuta maisha akiwa na wenzake watatu, lakini wenzake walifanikiwa
kurejea na yeye kukamatwa na kuwekwa mahabusu katika moja ya magereza
nchini humo.
“Ni mdogo wangu wa tatu, alikwenda Iran kutafuta maisha akiwa na wenzake
watatu, mmoja wa wenzake hao anaitwa Chalula, yeye ndiye aliyeleta taarifa kuwa
Ali amekamatwa na yuko gerezani,” alisema Balushi.
Alisema, walikwenda mara kwa mara katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa kufuatilia suala hilo, lakini waliishia kuambiwa waandike
barua yenye maelezo yanayoonyesha ndugu zao wamekamatwa kwa makosa yapi.
Alisema kwa mara ya kwanza walifikia Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa idara ya Mashariki ya Kati mwaka jana, na kukutana na
Hellen Kafumba aliyewaambia waandike barua ya maelezo kuhusu ndugu zao hao
waliokamatwa nchini Iran.
Aliongeza kuwa mara baada ya kuandika barua hiyo walijibiwa kuwa wasubiri
wizara inalishughulikia suala hilo.
Alieleza kuwa walisubiri kwa kipindi kirefu bila kupata majibu ndipo waliporudi
na wakapelekwa kwa mtu mwingine itwaye Kambona na kuambiwa kuwa mkakati uliopo
kwa sasa ni mazungumzo ya kubadilishana wafungwa yanaendelea.
Moja ya chanzo cha habari ambacho NIPASHE imekipata kutoka ubalozi wa Iran
nchini, zinasema kuwa Watanzania wengi hufika ubalozini hapo kuomba viza kwenda
Iran kuabudu katika moja ya makaburi waliozikwa wajukuu wa Mtume Muhamadi
(S.A.W) Hussein na Hassan yaliyopo katika mji wa Kerbala.
Habari zaidi zinaeleza kuwa wanapofika huko na muda wao wa kukaa ukiisha wengi
hujificha huko, hali inayopelekea kukamatwa.
Jitihada za kumpata msemaji wa ubalozi wa Iran nchini zilishindikana kutokana
na mwandishi kufika ubalozini mara kadhaa na kuambiwa kuwa hayupo.
Chanzo:
Nipashe





