Share this Post

dailyvideo

Mh.Zitto Zuberi Kabwe asema kwamba"Mabilioni ya Uswisi – Tusigeuzwe Mazezeta"



Jumanne tarehe 20 Novemba 2012, baadhi ya vyombo vya habari vimebeba habari
zinazohusu matamshi ya Waziri wa Utawala Bora ndugu George Mkuchika kuhusu
sakata ya mabilioni ya Uswisi. Waziri amesema kwamba Serikali ya Uswisi inataka
majina ya Watanzania walioficha fedha huko ndio waweze kusaidia uchunguzi.
Habari kama Hiyo, yenye maudhui na malengo hayo hayo iliandikwa na Gazeti la
The Guardian on Sunday la tarehe 18 Novemba 2012.
Nimeona ni vema nitoe kauli yangu rasmi kuhusu suala hili. Lengo ni kuweka rekodi
sawa juu ya Azimio la Bunge na kwamba Serikali inapaswa kutekeleza Azimio na sio
kutoa kauli tata za kukata tamaa.
Moja, Suala hili japo sio jipya lakini limeandikwa kama ni jambo jipya. Suala la
Serikali ya Uswisi kutaka majina lilisemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati
akichangia hoja binafsi niliyowasilisha Bungeni na pia wakati akileta maombi yake ya
kuiondoa hoja ambayo yalikataliwa na Bunge. Kama sio sababu mpya ni kwanini
imeibuka upya na kwa kasi? Ni wazi Serikali inajihami kwa kuona kuwa itashindwa
kutekeleza azimio la Bunge. Watanzania wasikubali propaganda hii ya Serikali.
Bunge limeagiza Serikali kufanya uchunguzi kwa kutumia njia za kiserikali au
wachunguzi binafsi wa kimataifa. Kwa nini Serikali inaanza kubwabwaja ilhali wala
haijaanza kazi hiyo? Serikali inajaribu kuficha nini? Kwa nini baada ya wiki iliyopita
Benki Kuu kufanya uchunguzi kwenye Mabenki ya Biashara jijini Dar es Salaam na
namna fedha zimekuwa zikipelekwa nje (international transfers), leo Serikali inakuja
na kauli za kukakata tamaa? Kunani?
Pili, Watanzania wajue kwamba Taifa la Swiss limejengwa na linajengwa kwa fedha
hizi za wizi ambazo watu mbalimbali duniani wanaiba au kukwepa kodi kwenye nchi
zao na kuzificha huko. Serikali ya Swiss hata siku moja haiwezi kutoa ushirikiano
kwa Serikali ya Tanzania katika suala kama hili. Ndio maana Azimio la Bunge
linataka wachunguzi binafsi ambao hawatahitaji ushirikiano wa Serikali ya Swiss.
Nawakumbusha kwamba mwaka 1997 mara baada ya Joseph Desire Mobutu
kuangushwa na Rais Joseph Kabila kule Kongo - Kinshasa, Serikali ya Swiss iliitaka
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuonyesha ushahidi kuwa hela hizo
za Mobutu zilikuwa zimepatikana kwa njia haramu! Waswiss walitaka Kabila
awakakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola bilioni nane za Kimarekani Mobutu
hakuzipata kihalali ndio waweze kuzirejesha. Zaire ilikadiriwa kuwa na zaidi ya dola
za Kimarekani bilioni thelathini katika Mabenki ya nje ya nchi hiyo. Majibu ya aina
aina hii ni majibu ‘standard’ ambayo kila nchi inapewa. Hata Marekani ilipokuwa
inafuatilia wakwepa kodi wao walijibiwa hivi hivi. Hatimaye Serikali ya Marekani
ikaamua kununua taarifa hizo na kuwakamata wakwepaji kodi wao walioficha fedha
Uswisi. Hao ndio Waswiss ambao Serikali ya Tanzania inashabikia majibu yao. Bila
Aibu Mawaziri wetu wanayanukuu majibu ya Waswiss kama kasuku. Tunasahau
historia haraka sana. Tunakuwa kama mazezeta.
Tusiwe Taifa la mazezeta. Mabwege na mazezeta huimba kila wanachoambiwa
kuimba. Sasa Serikali ya Tanzania imekuwa msemaji wa Serikali ya Swiss badala ya
kuchunguza utoroshaji wa fedha haramu na kisha kutoa taarifa Bungeni. Naitaka
Serikali ianze uchunguzi mara moja kama namna ilivyoelekezwa na Bunge. Suala hili
sio suala la kisiasa, sasa ni Azimio la Bunge ambalo linahitaji kutekelezwa kikamilifu.
Suala hili sio suala la Zitto Kabwe tena, ni suala la Bunge, ni suala la Wananchi.
Wananchi hawataki uzezeta wa watu waliopewa dhamana ya kutekeleza Azimio lao.
Kama hawawezi wapishe watu wenye uwezo wa kusimamia maslahi ya Watanzania
kwa kuchukua hatua stahili za kuchunguza utoroshaji mkubwa wa fedha za kigeni,
ukwepaji mkubwa wa kodi na ufisadi uliopelekea Watanzania kuficha mabilioni
kwenye mabenki nje ya Tanzania. Hatutakaa kimya mpaka tuone mwisho kamilifu wa
suala hili. Utekelezaji wa Azimio la Bunge itakuwa ni salamu tosha mafisadi na
watoroshaji wa fedha haramu kwamba hawana pa kujificha na Tanzania sio Taifa la
kuchezeachezea. Lazima tushinde vita hii. Anayeona hawezi kutuongoza kuishinda
atupishe mapema. Hatupaswi kuwa Taifa la Mazezeta. Watanzania sio mabwege
tena, Mwakyembe alipata kusema.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini.

Posted by Editor on 18:36. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for Mh.Zitto Zuberi Kabwe asema kwamba"Mabilioni ya Uswisi – Tusigeuzwe Mazezeta"

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery