Share this Post

dailyvideo

Simu bei 'bure' Soma hapa!

  TCRA yashusha panga kali
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma
Gharama za kupiga simu kutoka mtandao wa kampuni moja ya simu za mikononi kwenda mwingine nchini kuanzia Machi Mosi, mwaka huu, zitashuka kutoka Sh. 115 hadi Sh. 34.92 kwa dakika moja. Uamuzi huo umefanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) baada ya kufanya mapitio ya gharama za mwingiliano kwa kampuni za simu nchini wa mwaka 2013, pia kuanzia Januari Mosi, mwakani, gharama hizo zitapungua hadi Sh. 32.40. Vilevile, Januari, 2015 gharama hizo zitashuka hadi Sh. 30.58; Januari, 2016 zitashuka hadi Sh. 28.57 na Januari, 2017 zitashuka hadi Sh. 26.96 kwa dakika moja.  Akitangaza uamuzi huo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, alisema umetolewa kwa mujibu wa sheria ya TCRA ya mwaka 2003 Sura 172. Profesa Nkoma alisema viwango hivyo ni vya kikomo cha juu na pia ni elekezi, lakini akasema kampuni za simu zina uhuru wa kukubaliana kibiashara ili mradi makubaliano yao yasizidi gharama zilizoelekezwa na TCRA. Alisema gharama hizo zitatumika kwa mawasiliano ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na simu za kimataifa zinazoingia katika mitandao nchini. Hivyo, ameziagiza kampuni zote za simu kufanya makubaliano mapya baina yao na kuwasilisha nakala ya makubaliano kwa TCRA ifikapo Machi 31, mwaka huu. Alisema gharama hizo zimeshushwa ili kuwafanya watumiaji wa simu kuwa huru kupiga simu kwenda mtandao wa kampuni yoyote ya simu na kuwaondolea mzigo wa kubeba ‘laini’ nyingi za mitandao tofauti ya simu kwa wakati mmoja. Pia alisema ana imani kuwa uchangiaji wa matumizi ya miundombinu na matumizi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (Ucaf) na mkongo wa taifa wa mawasiliano, ndiyo suluhisho la kushuka kwa gharama za uendeshaji na kuenea kwa mawasiliano vijijini. Alisema watumiaji wa simu za mikononi wamekuwa wakilazimika kubeba ‘laini’ za mitandao tofauti, ambazo kila moja huitumia kupiga simu kwenda kwenye mtandao unaofanana nayo.  Profesa Nkoma alisema wamekuwa wakifanya hivyo ili kukwepa kutozwa gharama kubwa za kupiga simu kutoka mtandao mmoja wa simu za mikononi kwenda mwingine.  Alisema uamuzi wa kushusha gharama za mwingiliano wa mawasiliano ya simu za mikononi utakuwa sheria, ambayo kampuni zote za simu zitalazimika kutii.  “Sasa hivi tuna mitandao kama saba ya simu. Ni bughudha kwa wananchi kutembea na mzigo wa ‘sim card’ (‘laini’) ili kukwepa gharama za kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine,” alisema Profesa Nkoma na kuongeza:  “Sisi kama mdhibiti tunaona hali hii si nzuri. Tunataka mtu awe huru kupiga simu mtandao wowote.”  Hata hivyo, alisema kama itatokea sababu ya bei hizo kuangaliwa upya, TCRA itafanya hivyo.  Alisema suala la kushuka kwa gharama za mwingiliano wa mawasiliano ya simu kutoka mtandao wa kampuni moja kwenda mwingine, hivi sasa linatumika duniani kote, zikiwamo nchi jirani, kama vile Kenya, Uganda na Rwanda.  Profesa Nkoma alisema tofauti na nchi kama vile Marekani na Canada, gharama za Tanzania za mwingiliano wa mawasiliano ya simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine zimelingana sawia na zile za Uganda.  Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, jopo la udadisi lilianza kazi yake Desemba 17, mwaka jana hadi Janauri 28, mwaka huu.   Profesa Nkoma alisema jopo hilo lilizingatia pamoja na mambo mengine ripoti ya mtaalamu elekezi, PriceWater House Coopers (UK) LLP, ambaye alifanya mchanganuo wa gharama halisi za utoaji huduma zinazowiana na gharama za mwingiliano kati ya mitandao ya simu nchini.  Alisema katika utafiti wake, mtaalamu elekezi alizingatia na kutumia mfumo wa ongezeko au kupungua kwa gharama kwa miaka ya mbele (FL-LRIC).  Profesa Nkoma alisema jopo hilo lililoteuliwa na TCRA, liliwasilisha ripoti yake Januari mwaka huu.  Kutokana na hali hiyo, alisema uamuzi huo utajulikana kama uamuzi namba tatu wa mwaka 2013 kuhusu bei za mwingiliano wa mintandao ya simu inayoyozingatia gharama halisi  na ufanisi.  Alisema uamuzi huo utaanza kutumika Machi Mosi, mwaka huu kwa mitandao yote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya uamuzi namba mbili wa mwaka 2007 uliotolewa na mamlaka kufikia kikomo Februari 28, mwaka huu.  Profesa Nkoma alisema udadisi ulifanyika kwa uwazi kwa kuhusisha kampuni zote za simu na wadau wengine, wakiwamo wananchi kwa mujibu wa sheria ya TCRA na mwongozo wa udadisi wa 2004. Alisema udadisi ulizingatia upekuzi wa maandiko, miongozo, kuhoji wadau, mawasilisho katika maandishi, maoni katika mkutano wa pamoja wa wadau na wananchi, watumiaji, wataalamu kutoka serikalini na umma kwa jumla.  Profesa Nkoma alisema mwisho wa yote jopo lilitayarisha ripoti na kuiwasilisha kwa mamlaka Janauri 28, mwaka huu.  Alisema jopo lilithibitisha katika udadisi kwamba, kampuni zote za simu kwa jumla zinakubaliana kwamba, gharama za mwiangiliano za sasa ziko juu na zinatakiwa kupungua; lakini wanatofautiana katika kiwango, ambacho wangependa kishushwe. “Mamlaka inakubaliana na maoni ya jopo yaliyotokana na udadisi kwamba gharama za mwingiliano kwa sasa ziko juu na zinahitaji kushuswa kwa kuzingatia gharama halisi ya utoaji huduma,” alisema Profesa Nkoma. Alisema TCRA imejiridhisha kuwa ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na mtaalamu elekezi katika ripoti yake ya gharama za mwingiliano ya 2012 yanakubalika kwa kuzingatia hali halisi ya soko la huduma za simu kwa wakati huu. Pia alisema TCRA imejiridhisha pia kuwa kigezo alichotumia kwa kuangalia ongezeko au kupungua kwa gharama siku za usoni inakubalika kimataifa na pia inazingatiwa katika sheria zinazosimamia sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) nchini.  Alisema TCRA pia inakubaliana na gharama za wastani wa gharama za mtaji za jumla wa asilimia 22.88 iliyotumika na mtaalamu elekezi kama kigezo cha gharama halisi. Pia gharama alizotumia kama kigezo, zilizingatia mazingira halisi ya soko na uchumi wa Tanzania, ikiwamo makadirio ya mfumko wa bei wa muda mrefu unaotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hatari katika nchi na uwekezaji, riba, kodi, ambazo jopo la udadisi limeyazingatia pia. Alisema TCRA imegundua na kuthibitisha kuwa gharama za mwingiliano zimepungua sana katika nchi nyingi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Profesa Nkoma alisema kiwango kinachotumika Tanzania kwa sasa ni juu ukilinganisha na baadhi ya nchi za Afrika. Alisema TCRA inakubaliana na jopo la wadadisi kuwa kila kampuni ina ukiritimba katika gharama za mwingiliano kwa sasa kwa simu zinazoingia katika mitandao yao kutoka mitandao mingine.    “Kwa sababu hiyo basi, Mamlaka inalazimika kudhibiti gharama hizi ili kukuza ushindani na soko,” alisema Profesa Nkoma. Hata hivyo, alisema TCRA inatambua kuwa kwa kipindi kifupi kutakuwa na upungufu wa mapato kwa baadhi ya kampuni, ambazo zilikuwa zinategemea kwa kiasi kikubwa gharama za mwingiliano kama sehemu ya mapato.  “Ila kwa upande wa makampuni yaliyokuwa yanalipa zaidi, gharama zake za uendeshaji zitapungua kwa kuwa malipo kwa makampuni mengine yatapungua,” alisema Profesa Nkoma na kuongeza: Alisema TCRA inakubaliana na jopo la wadadisi, baadhi ya kampuni za simu na wadau mbalimbali waliotoa maoni yao kuwa kushuka kwa gharama za mwingiliano katika huduma za simu ni lazima na itawezesha kushuka kwa gharama za rejareja kwa wateja kwa kupiga mitandao mbalimbali. Hata hivyo, alisema TCRA haikubaliani na maoni ya baadhi ya kampuni za simu kwamba, kushushwa kwa gharama hizo kutazorotesha upanuzi wa huduma za mawasiliano vijijini kwa sababu havihusiani.  Alisema gharama za mwingiliano kazi yake ni kumrudishia mtoa huduma gharama za kufikisha mawasiliano kwa mwingine tu na si vinginevyo. Profesa Nkoma alisema TCRA inakubaliana na maoni ya jopo la udadisi kuwa soko lina ushindani mkali na linabadilika kwa kasi, kama ambavyo inajidhihirisha katika huduma mpya zinazotolewa kila wakati.  Alisema TCRA inakubaliana na jopo la udadisi katika maoni yao kuwa soko la simu za kimataifa lina ushidani wa kutosha kwa kuwapo watoa huduma wa simu za kimataifa wengi.  
CHANZO: NIPASHE

Posted by Editor on 13:37. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for Simu bei 'bure' Soma hapa!

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery