AUNT EZEKIEL AONGEA NA BODI YA FILAMU TANZANIA
Wasanii
nchini wameshauri kuwa na imani na Bodi ya Filamu na kuondokana na
dhana potofu iliyojengeka juu ya Bodi hiyo kuwa haipo rafiki na
wasanii.
Hayo
yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Msanii wa Filamu za Kiswahili
Aunty Ezekiel katika kikao na Bodi ya Filamu wakati wa kupitia maeneo
yaliyohitaji marekebisho kwa filamu yake mpya ya “Scola”.
Aunt
Ezekiel ameeleza kuwa amefurahishwa na Bodi ya Filamu Tanzania kwa
kufanya majadiliano mazuri juu ya filamu yake kwa kubaini mapungufu
baadhi yaliyopo na kumuelekeza cha kufanya.
Aunt
Ezekiel amesema “Nashukuru bodi wamekuwa waelewa, wamenielekeza
kurekebisha baadhi ya vipengele ili kuboresha filamu yangu na naahidi
kuirekebisha kwani vinarekebishika”.
Aidha
Aunt Ezekiel ameomba radhi kwa kutoleta script yake ya filamu hiyo mpya
ya SCOLA kwa Bodi ya Filamu na amesema atakuwa akiwasilisha miswada
yake kabla ya kutengeneza filamu zake.
Aidha amewahakikishia watanzania kuwa atakuwa mfano bora katika kutengeza filamu bora na zenye maadili.
Kwa
upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi hiyo Bi. Joyce Fissoo ameeleza
kuwa kuna umuhimu wa wasanii kufuata sheria na taratibu za filamu kabla
ya kuanza kutengeneza na kuzitoa filamu zao, ambapo sheria inawataka
kuwasilisha mswada (script) Bodi ili kupewa idhini ya kuendelea na kazi
hiyo.
“Wasanii
mnatakiwa kuzingatia sheria na kuwasilisha script ili zikaguliwe na
kupata ruhusa kwa mujibu na taratibu za sheria kabla ya kuanza
kutengeneza filamu kwa sababu sheria Na 4 ya mwaka 1976 ya Filamu na
Michezo ya kuigiza pamoja na kanuni zake, zinaelekeza wasanii kutotoa au
kutengeneza filamu kabla ya kupeleka mswada (script ) Bodi ya Filamu
ili ipitiwe.
Aidha
Katibu huyo amefafanua kuwa wasanii wanapotengeneza filamu kupitia
script ambazo hazijakaguliwa, kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo sehemu
ambazo zinakiuka maadili ya mtanzania, ikiwepo uvaaji wa mavazi mafupi
yaliyopitiliza kwa waigizaji wanawake, lugha mbaya na baadhi ya vitendo
vingine visivyofaa kuoneshwa kwa umma.
Amewataka
wasanii nchini kutengeneza filamu zinazozingatia maadili ya Kitanzania
ikiwemo kutocheza picha zenye mavazi yanayoopitiliza kwa ufupi, kubana
au zinazoonesha maumbile ya muigizaji mara kwa mara.
Kikao
hiki pia kiliwashauri Bodi ya Filamu kukutana na wasnii wa kike ili
kujadili masuala ya mavazi yasiyo na staha, Bodi imeridhia ombi hilo.





