SOMA TAARIFA YA KAMATI KUHUSU KUWASILI KWA MWILI WA MAREHEMU MANGWEA.
KAMATI
ya Mazishi ya aliyekuwa Msanii wa Bongo Fleva, Albert Mangwea ‘Ngwea’,
mpaka jana mchana ilikuwa imekusanya jumla ya Sh milioni 32 kutoka kwa
wadau mbalimbali.
Kamati
hiyo inahitaji Sh milioni 50 kwa ajili ya kusaidia kusafirisha mwili wa
marehemu kutoka Afrika Kusini mpaka Morogoro kwa ajili ya mazishi. Fedha
hizo pia zinahitajika kwa ajili ya kuratibu shughuli nzima ya mazishi.
Mangwea
alifariki dunia Jumanne iliyopita nchini Afrika Kusini akiwa usingizini
kwa madai ya kuzidisha matumizi ya madawa ya kulevya.
Alitarajiwa
kuwasili nchini jana lakini kushindwa kutoka kwa ripoti ya uchunguzi wa
madaktari kwa wakati, kumesababisha isijulikane atatua lini, licha ya
kudaiwa kuwa anaweza kutua leo.
Kamati ya Mazishi bado inaendelea na mchakato wa kuratibu shughuli hiyo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na mwandishi wetu akiwa Mbezi Goig jijini Dar ambako ndiko kwenye msiba
huo, mmoja wa waweka hazina wa kamati hiyo, Paul Matthysse ‘P-Funk’,
alisema mpaka sasa kamati yake imefikisha Sh 32,259,000 ingawa
wanatarajia kuendelea kupokea michango mbalimbali kutoka kwa wadau.
Miongoni
mwa watu wa kwanza kutoa michango yao katika msiba huo ni P-Funk
aliyetoa Sh milioni tano, Clouds Media Group (Sh milioni tano) na Push
Mobile (Sh milioni tano).
Juzi Kampuni ya Global Publishers ilitoa Sh milioni moja.
“Nawasisitiza
Watanzania waendelee kutoa michango yao kwa ndugu yao ili kuonyesha
umoja tulionao. Fedha zikiwa nyingi tunataka kumfanyia kitu mama yake
ili kuendelea kumfariji kwani kipindi hiki ni kigumu kwake,” alisema
P-Funk.
Wakati
huohuo jana taarifa zilisema mama mzazi wa Mangwea aishie Morogoro,
Denisia Mangwea, alipandwa na presha baada ya jana kupata taarifa kuwa
mwili wa mwanaye umezuiwa Afrika Kusini kutokana na uchunguzi wa madawa
ya kulevya. Alikimbizwa hospitali na inadaiwa anaendelea vizuri.
Mangwea aliwahi kutamba na nyimbo kadhaa kali zikiwemo Gheto Langu, She Got a Gwan, Mikasi na Tupo Juu.




