Share this Post

dailyvideo

Just in: Msanii wa Filamu Elizabeth Kimemeta a.k.a Lulu kuanza kujibu mashtaka ya kumuua bila kukusudia Steven Kanumba Februari 17


Msanii wa filamu Elizabeth Michael Kimemeta (18), maarufu kama Lulu (pichani) anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya bila kukusudia ya msanii mwenzake Steven Kanumba (28), anatarajia kujibu mashitaka yake kwa mara ya kwanza Februari 17, mwaka huu katika Mahakakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam. Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya kesi za mauaji na bila kukusudia, iliyotolewa na Mahakama Kuu kwa kanda hiyo, kesi ya Lulu itasikiliza mbele ya Jaji Rose Teemba na mshtakiwa atajibu mashitaka yake kama ni kweli au siyo kweli.Aidha ratiba hiyo inaonyesha kwamba mshtakiwa akisomewa mashtaka na kujibu, mahakama itapanga tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali dhidi ya kesi hiyo.
Mnamo Januari 29, mwaka 2013 Lulu aliachiwa kwa dhamana baada ya kesi hiyo kubadilishwa hati ya mashitaka kutoka kwenye kesi ya mauaji kwenda mauaji ya bila kukusudia.
 Aidha, Lulu alipata dhamana hiyo baada ya Jaji Zainabu Mruke kutoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo baada ya wakili wa utetezi Peter Kibatala kuwasilisha maombi ya dhamana kwa hati ya dharula chini ya kifungu cha 148 kidogo cha (1) na cha (2) cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA).   Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Joseph Maugo na Kishenyi Mutalemwa.
 Wakili Kibatala alidai kuwa hati hiyo imeambatanishwa na hati ya mashtaka yanayomkabili Lulu la kuua bila kukusudia na kwamba kwa mujibu wa shtaka hilo mshtakiwa ana haki ya kupata dhamana.
 Upande wa Jamhuri, ulidai kuwa hauna pingamizi la maombi hayo na kwamba mahakama ijielekeze kwenye kifungu cha 148 kidogo cha (6)ambacho kinamtaka mshtakiwa kufuata masharti yatakayotolewa chini ya kifungu hicho.
 Jaji Mruke alisema kosa linalomkabili mshakiwa lina dhamana kisheria na kwamba mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kufuata masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 20 kila mmoja.
"Tukubaliane wote kwamba hakuna ubishi roho ya mtu imepotea hivyo sheria lazima ifuatwe... pia mshtakiwa awasilishe hati zake za kusafiria, kuripoti kila tarehe Mosi ya mwezi kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, asitoke nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha msajili huyo" alisema Jaji Mruke.
 Alisema Msajili wa Kanda ya Dar es Salaam ahakiki masharti ya dhamana kabla ya mshtakiwa hajaachiwa kwa dhamana.
 Katika kesi ya msingi, Lulu anadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alimuua Kanumba bila kukusudia.
MICHUZI MEDIA GROUP

Posted by Editor on 17:20. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for Just in: Msanii wa Filamu Elizabeth Kimemeta a.k.a Lulu kuanza kujibu mashtaka ya kumuua bila kukusudia Steven Kanumba Februari 17

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery