Share this Post

dailyvideo

Dola milioni 35 kugombaniwa fainali


Bingwa mara tatu Ujerumani na bingwa mara mbili Argentina zitagombania dola milioni 35 kwenye mechi ya fainali ya kombe la dunia Jumapili Julai tarehe 13 mjini Rio De Janeiro.
Shirikisho la kimataifa Fifa limetoa jumla ya dola milioni 576 kushindaniwa kwenye mashindano ya mwaka huu nchini Brazil.
Mshindi ataweka kibindoni dola milioni 35 na wa pili $25 milioni, wa tatu $22milioni wa nne $20 milioni.
Timu nne zilizoondolewa kwenye robo-fainali zitapokea $14 milioni kila mmoja, timu nane zilizong'olewa raundi ya pili $9 milioni na timu 16 zilizoondolewa raundi ya kwanza $8 milioni kila mmoja.
Ujerumani imefuzu kwa fainali baada ya kuiadhibu Brazil mabao 7-1 na Argentina ikaiondoa Uholanzi mabao 4-2 ya penalti mechi ya nusu-fainali. Kwa jumla timu 32 zimeshiriki mashindano ya mwaka huu kwenye mechi 64 na wachezaji 736 wakajitosa uwanjani.
Argentina ilifuzu baada ya kushinda Uholanzi
Miongoni mwa wachezaji nyota kwa upande wa Ujerumani ni mfungaji bora zaidi kwenye mashindano haya Miroslav Klose huku Argentina ikijivunia Lionel Messi mshindi wa tuzo la mchezaji bora duniani mara nne.
Hii ni mara ya tatu Ujerumani na Argentina wanakutana fainali ya kombe la dunia, mara ya kwanza ikiwa mwaka wa 1986 nchini Mexico Argentina ikashinda 3-2 kisha wakapatana tena mwaka wa 1990 nchini Italia na Ujerumani ikalipiza kisasi kwa kuinyoa Argentina bao 1-0.
Wadadisi wengi wa kandanda wanasema Ujerumani wana nafasi nzuri zaidi ya kuibuka mshindi kwani wameonyesha kiwango cha juu zaidi ya Argentina kufikia sasa.
Lakini mpira unadunda hivyo basi Argentina nao pia waeza kuibuka mshindi ikikumbukwa kwamba hamna timu ya bara Ulaya imewahi kunyakua ubingwa wa dunia mashindano haya yakifanyika Marekani Kusini.
Kwa jumla mataifa ya Marekani Kusini yameibuka mshindi mara tisa kwenye kombe la dunia na ya Ulaya mara kumi Italia na Ujerumani wakiongoza kwa kushinda mara tatu kila mmoja na Brazil ikiwa juu Marekani Kusini kwa kushinda mara tano, Argentina na Uruguay mara mbili kila mmoja.
 BBC NEWS
Ikiwa unatukio Lolote au Habari yoyote usisite kututumia kupitia Barua Pepe blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba yetu +255765056399

Posted by Editor on 17:35. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for Dola milioni 35 kugombaniwa fainali

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery