KISWAHILI KUWA LUGHA RASMI EAC
UONGOZI wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) umesema, kuna mipango ya
kukifanya Kiswahili iwe lugha rasmi ya jumuia hiyo yenye watu zaidi
milioni 150.
Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko ameyasema hayo wakati
alipokuwa anazungumza na Balozi mpya wa Uganda nchini Tanzania, Richard
Kabonero kwenye ofisi za makao makuu jijini Arusha hivi karibuni. Hadi
sasa Kiswahili ni lugha ya Taifa nchini Tanzania na baadhi ya wananchi
kwenye nchi nyingine wanachama wanaizungumza lugha hiyo.
Hivi karibuni Naibu Waziri Mkuu wa Uganda anayeshughulikia masuala ya
EAC, Kirunda Kivejinja alisisitiza umuhimu wa wananchi kwenye nchi
wanachama kukitumia Kiswahili kuwaunganisha. Kiongozi huyo ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri EAC alisema, nchi wanachama wa EAC
hazitafanikiwa kutekeleza kifungu cha 137 (2) cha makubaliano ya
kuanzishwa jumuia hiyo kama hazitakitumia Kiswahili kuwaunganisha.
Aliyasema hayo Zanzibar wakati wa hafla ya kufungwa kwa Mkutano wa
kwanza wa Kimataifa ulioandaliwa na Tume ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki (EAKC). Alisema ni muhimu kwa Kiswahili kifanywe rahisi na
sehemu kubwa ya watu kwenye eneo la EAC waitumie lugha hiyo na lugha zao
za asili zikiwemo za zaidi ya makabila 120 nchini Tanzania. Alitoa
pendekezo kwa EAKC kutoa mapendekezo kwamba Kiswahili kitumike vipi ili
kufanikiwa katika utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs).
Katibu Mkuu wa EAKC, Profesa Kenneth Simala alisema kwenye mkutano
huo kuwa, tume hiyo inafanya kazi kwa karibu na vyama vya Kiswahili
kwenye nchi wanachama ili viwe na umoja. Wajumbe wa mkutano huo
walijadili, pamoja na mambo mengine namna Kiswahili kinavyoweza kutumika
kuzidisha mtangamano EAC sanjari na kuchangia utekelezaji wa malengo
endelevu.
Wajumbe walieleza umuhimu wa kuanzishwa haraka mabaraza ya Kiswahili
na vyama vya lugha hiyo kwenye kila nchi, kutumia lugha hiyo kwenye
ngazi mbalimbali za elimu, kuhamasisha tafiti za Kiswahili na nchi
wanachama kuitumia lugha hiyo kwenye programu za elimu ya watu wazima.
Wakati wa mazungumzo na Balozi Kabonero jijini Arusha, Balozi
Mfumukeko alisema, pamoja na suala hilo la lugha ya Kiswahili, EAC pia
inajielekeza kwenye kuongeza uwekezaji kwenye viwanda na sekta ya kilimo
ikiwa ni sehemu ya mikakati kupunguza ukubwa wa tatizo la ukosefu wa
ajira. Alisema, licha ya kutekeleza protokali za ushuru wa pamoja wa
forodha, soko la pamoja na fedha ya pamoja, jumuiya pia inatafuta
rasilimali ili kutekeleza miradi ya maendeleo ya miundombinu zikiwemo
reli na barabara.
CHANZO HABARI LEO
Posted by Editor
on 12:13.
Filed under
eastafricannews,
gallery
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0