MKURUGENZI MKUU WA FAO KUZURU TANZANIA, KUFANYA MAQZUNGUMZO NA VIONGOZI WAANDAMIZI WA SERIKALI, WADAU
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la
Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva(pichani), Jumanne wiki hii ataanza ziara
rasmi nchini Tanzania ambapo anategemewa kufanya mikutano na mazungumzo na
maofisa waandamizi wa serikali na wadau.
Bw. Graziano da Silva anategemewa kukutana na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO amepanga kufanya mikutano na
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Tanzania Bara), Dkt. Charles Tizeba, na
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed.
Ziara hii ya Mkurugenzi Mkuu inakuta wakati FAO ikiadhimisha
miaka 40 toka kuanza shughuli zake hapa Tanzania. Wakati wa ziara hii, Bw. Graziano
da Silva atakutana na uongozi na wafanyakazi wa FAO hapa Tanzania kabla ya
kuhudhuria hafla maalum hapa Dar es Salaam kusherehekea maadimisho hayo. Hafla
hiyo itahudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Samia
Suluhu Hassan.
Mwakilishi Mkazi wa FAO hapa nchini, Bw. Fred
Kafeero, amethibitisha kuwa Bw. Graziano
da Silva atakuwa hapa nchini kufuatia mwaliko wa Serikali ya Tanzania. “Mkurugenzi
Mkuu wa FAO atabadilishana mawazo na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwenye
masuala makuu yanayohusiana na uhakika wa chakula na maendeleo ya kilimo,
ikijumuisha juhudi za FAO kitaifa na kikanda,” alisema. Bw. Graziano da Silva pia
atajadili mambo mengine yanayohusiana na ushirikiano kati ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na FAO, pia masuala mengine ya umuhimu kati ya pande hizo
mbili, aliongeza. Mbali ya Maafisa wa Serikali, Mkurugenzi Mkuu atakutana na
wadau wengine wa FAO hapa nchini wakiwa ni pamoja na asasi za kiraia, taasisi
za elimu, na taasisi za utafiti.
Baadae Mkurugenzi Mkuu ataenda Zanzibar ambapo,
miongoni mwa mambo mengine, anategemewa kuweka jiwe la msingi katika jingo la
Mradi wa Kuzalisha vifaranga vya samaki unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya
Korea kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa KOICA. Pia Bw. Graziano da Silva atapata fursa ya
kutembelea mradi wa kilimo cha mwani na pia kuona maonesho ya bidhaa mbali
mbali zilizotengenezwa na wanawake wanaojihusisha na kilimo cha mwani.
Tanzania ilijiunga na FAO mwaka 1962, na mwaka 1977
FAO ilifungua ofisi zake hapa Tanzania. Katika miaka 40 ya uwepo wake, FAO imeisadia
Serikali ya Tanzania katika kupanga na kutekeleza sera, mikakati na mipango ya
kilimo hapa nchini. Kazi ya FAO imejikita katika kuboresha usalama wa chakula
na lishe pamoja na maisha ya wakulima wadogo na hivyo kuwa chachu ya kukua kwa
uchumi kupitia sekta ya kilimo.
Posted by Editor
on 14:04.
Filed under
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0