KASHFA YA MABILIONI KUFICHWA USWISI: Watanzania 27 wahusika
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo wengine wanne, ambapo anayefuatia anamiliki Dola 30 milioni (Sh48 bilioni), mwingine Dola 20 milioni (Sh32 bilioni) na wengine wawili kila mmoja anamiliki Dola 10 milioni (Sh16 bilioni). Kwa kuangalia fedha hizo ni dhahiri kwamba vigogo watano tu kati ya kundi la Watanzania 27, wanamiliki Dola 126 milioni (Sh201.6 bilioni) sawa na asilimia 67.74 ya fedha hizo, wakati wengine 22 waliobaki wanamiliki Dola 60 milioni (Sh96 bilioni) sawa na asilimia 32.25.
Kwa hesabu za kawaida, kiasi cha Sh300 bilioni, kinaweza kugharimia ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 33,300, ikiwa chumba kimoja kinaghirimu kiasi cha Sh9 milioni.
Katika orodha ya walioweka fedha nchini humo, pia wamo wafanyabiashara wanaomiliki kiasi cha dola kati ya milioni mbili na milioni saba. Kadhalika wamo wawili waliowahi kuwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, ambao akaunti zao zina kiasi kisichozidi Dola 500,000 kwa kila mmoja.
Kashfa ya kuwapo kwa vigogo walioficha fedha zao nchini Uswisi iliibuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini mwezi Juni mwaka huu, na baadaye mwangwi wake kulitikisa Bunge katika mkutano wake wa nane uliomalizika juzi mjini Dodoma.
Habari hizo zilikuwa zikinukuu taarifa ya Benki Kuu ya Uswisi iliyoitoa na kuonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa Tanzania na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Jumatano wiki hii, tuhuma hizo ziliibuka bungeni ambapo Kambi ya Upinzani ilidai kwamba inawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja ikiwa Serikali haitawataja.
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe alipokuwa akiwasilisha hotuba ya kambi yake kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha na Uchumi alisema, miongoni mwa wanaomiliki fedha hizo ni kiongozi wa juu nchini pamoja na aliyepata kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa.
“Kambi ya Upinzani bungeni imepata taarifa mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa Tanzania na baadhi ya mawaziri wa awamu zilizopita ni miongoni mwa watu wenye fedha hizi,” alisema Zitto huku akiitaka Serikali kuliambia taifa ni hatua gani itakazochukua kurejesha fedha hizo pia kuwataja wamiliki wake.
Baada ya Zitto kumaliza kuwasilisha hotuba yake, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole-Sendeka aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala hilo, akisema kuwa tuhuma hizo ni nzito, hivyo kumwomba Naibu Spika, Job Ndugai amtake kutoa ufafanuzi ama ikiwezekana kuwataja wahusika.
Hata hivyo, Ndugai baadaye alisema taarifa hizo ni za uongo na uzushi kwani Zitto hakuwa na ushahidi wa kuthibitisha kauli yake wala kuwataja wahusika kama ambavyo alidai, huku akimtuhumu kwamba anautumia vibaya Ukumbi wa Bunge kwa kutoa tuhuma nzito bila kuzifanyia utafiti.
Uchunguzi zaidi Katika hotuba yake bungeni, Zitto alidai kuwa fedha hizo zinatokana na biashara (deals) zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kwenye sekta za nishati na madini na kwamba sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika Pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kuwa fedha zilizopo kwenye akaunti za vigogo wanaohusishwa na ufisadi huo, mara ya mwisho ziliwekwa kwenye akaunti husika mwaka 2005.
Taarifa zaidi ambazo Mwananchi limezipata zinadai kuwa taarifa za kufichwa kwa mabilioni hayo ya shilingi nchini Uswisi zimekuwa zikipatikana kwa msaada wa Mbunge mmoja wa zamani wa Afrika Kusini, (jina tunalihifadhi kwa sasa).
Akizungumza jana Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) anasisitiza kuwa walioweka fedha hizo nchini Uswisi wanafahamika na kwamba ikiwa Serikali haitawataja na kuwachukulia hatua, wao (Chadema) watawataja wakati mwafaka ukifika.
“Kama nlivyowahi kusema, tufanye kama nchi ya India, wenzetu hawa walitangaza kwamba watu wote walioweka fedha nje ya nchi kwa njia isiyo halali, wazirejeshe. Walifanikiwa sana, na sisi tunapaswa kufuata nyayo hizo, fedha hizo tunazitaka ili zitusaidie katika kuendesha uchumi wetu,” alisema Zitto. Mwananchi
Posted by Editor
on 11:55.
Filed under
eastafricannews
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0