MICHUANO YA KOMBE LA TAIFA 2012 YAOTA MBAWA
Michuano ya Kombe la Taifa (Taifa Cup) inayoshirikisha kombaini za mikoa ya Tanzania Bara haitakuwepo mwaka huu kutokana na kukosekana kwa udhamini.
Licha ya kukosekana kwa udhamini, awali tulifikiria kuendesha mashindano hayo kwa michango ya wanachama wetu (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa) na Serikali za mikoa kugharamia timu zao.
Lakini baadhi ya wanachama wetu na Serikali za mikoa walitushauri kuwa ni ngumu kuendesha mashindano hayo kwa sasa kutokana na shughuli za kitaifa zinazoendelea hivi sasa ikiwemo maandalizi ya sensa ya watu na makazi.
Kwa mujibu wa Kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), mashindano ya Kombe la Taifa yalitakiwa kufanyika kuanzia Julai 23 hadi Agosti 6 mwaka huu.
Michuano ya Kombe la Taifa msimu uliopita ilidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambapo Mbeya iliibuka mabingwa katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.