Share this Post

dailyvideo

Serikali yaingilia kati mgogoro wa Chadema, CCM

 
Fredy  Azzah, Dar na Venace George, Kilosa
SERIKALI imesema  itafanya uchunguzi juu ya baadhi ya vyama vya siasa na wanasiasa wanaodaiwa kupata fedha chafu kutoka kwa taasisi na watu binafsi walio nje ya nchi.

Kauli hiyo imekuja baada ya  Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kukituhumu Chadema kwamba kinapewa fedha chafu  na wafadhili wa nje.

Wakati Nape akiibua tuhuma hizo, Katibu mkuu wa Chadema , Dk Willibroad Slaa wakati akihutubia    mkutano wa hadhara uliofanyika  jimbo la Kilosa mkoani Morogoro juzi jioni, alisema fedha chafu ndiyo zilizomuweka Nape madarakani.

Akizungumza wakati akijibu swali la Mbunge Jimbo la Nkasi Kaskazini kupitia (CCM), Ali Kessy aliyetaka kujua Serikali imejipanga vipi kudhibiti vyama na wanasiasa wanaopata fedha chafu kutoka nje ya nchi.


Kessy aliuliza swali hilo katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, ambapo alisema wezi wa magari na fedha chafu, sasa wameingia kwenye siasa na wanapata fedha hizo kutoka kwa watu binafsi na taasisi mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Swali hilo lilionekana kuilenga Chadema kwa kuwa Agosti 11 Chadema chama hicho kilifanya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendesha kampeni ya vuguvugu la mabadiliko (M4C).

Mara baada ya harambee hiyo, Nape alisema  Chadema kinafanya kampeni za kuchangisha fedha ikiwa ni  kuhalalisha mabilioni ya fedha wanazopewa na wafadhili wa nje ya nchi.

Alisema  mkakati huo unafanywa kwa siri na wafadhili hao kuchochea machafuko nchini ili wafaidi kirahisi raslimali za Tanzania kama vile madini, gesi na mafuta ambayo yamegundulika kuwepo nchini.

Kauli hiyo ya Nape iliifanya Chadema kupitia kwa  Mkurugenzi wake wa  Fedha na Utawala, Anthony Komu kushitaki  kwa  Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kumtaka Nape atoe maelezo juu ya madai yake.

Lakini jana, Pinda bila kutaja makundi hayo yanayolumbana, alisema serikali imepata taarifa hizo kupitia mtandao na imeamua kutozipuuzia na kuamuru vyombo vinavyo husika vifanye uchunguzi.

“Nadhani tuseme Serikali imejipanga kuchukua hatua stahiki gani, ni kweli kuna taarifa kama hizi kwenye mtandao, lakini tatizo langu ni kwa kiasi gani tunaweza kuziamini hizi taarifa kwa sababu hapa ni sehemu ambapo kila mtu anaweza kuandika kile anachojisikia,” alisema Pinda na kuongeza;

“Lakini tumeona tusizipuuze na tumeagiza vyombo vinavyohusika vizichunguze juu ya fedha hizo chafu.”

Nnauye akitoa tuhuma hizo alisema, CCM kimeshangazwa kuona Chadema kikiwahadaa Watanzania  kufanya harambee ili kuhalalisha fedha walizonazo kutoka kwa wafadhili.

 “Chama Cha Mapinduzi kimeshangazwa na kusikitishwa sana na usanii mkubwa unaofanywa na Chadema kwa kuwahadaa Watanzania kwa usanii wa kufanya harambee kuhalalisha uwepo wa mabilioni waliyopewa na wafadhili wao wa nje ya nchi.” 

Aliongeza; “Mfano mzuri wa usanii huu ni juzi  siku ya Ijumaa (Agosti 11) kwenye Hoteli ya Serena ambapo ilifanyika harambee na kurushwa moja kwa moja na kituo kimoja cha televisheni.”

Alisema CCM inao ushahidi wa kutosha unaoonyesha mabilioni waliyopewa Chadema na wafadhili kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuendeleza operesheni mbalimbali nchini. 

Alionya kuwa fedha hizo zinatokana na watu mbalimbali wanaomezea mate raslimali za Tanzania.
“Hebu tujiulize, kwa nini mabilioni haya yanatolewa kwa Chadema sasa ambapo nchi yetu imeendelea kufanya utafiti na ugunduzi wa rasilimali mbalimbali zikiwamo gesi na mafuta? 

 “Je, ufadhili huu kwa Chadema licha ya kufichwa sana na kufanywa siri, una nia njema kwa nchi yetu na rasilimali za nchi yetu? Kwanini ufadhili huu wa mabilioni unafanywa siri ya watu wachache hata ndani ya chama chenyewe?”

Kwa upande wa  Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Komu, akizungumza na gazeti hili kuhusu madai yaliyotolewa na Nnauye, alisema chama chake, hakijawahi kufadhiliwa na wahisani kutoka nje na kwamba  mapato yake yanatokana na ruzuku ya Sh235 milioni inayotolewa na Serikali kila mwezi.

Kauli ya Dk Slaa

Dk Slaa alisema Nape hana uhalali wa kufikiria kuwa kuna vyama vina takatisha fedha chafu kwa kupitia michango ya wananchi na badala yake anapaswa kuwaambia wana CCM  wenzake namna Chama hicho kilivyotumia fedha chafu kuingia madarakani mwaka 2005.

 “Nimemsika Nape akiendeleza madudu yaliyo kichwani mwake kuwa alikuwa anatoa tahadhari tu sasa ninamwambia Yule si saizi ya Chadema na Dk Slaa zaidi ninamkumbusha kuwa Fedha za Tangold, Kagoda na Meremeta ndizo zilizokiingiza chama chake madarakani hivyo awape tahadhari hao badala ya wananchi wanaokichangia Chadema kwa mioyo yao ya kutaka kujikomboa”alisema Dk Slaa

Alisema wameshamwandikia msajili wa vyama vya siasa amtake Nape na CCM wathibitishe namna Chadema inavyopata fedha chafu na kama ikishindikana basi jeshi la Polisi limchukulie hatua kwa kuwa ni kauli za uchochezi na chuki dhidi ya watanzania.

Aliongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona mkuu wa Polisi nchini IGP Said Mwema na timu yake wameshindwa kuchukua hatua za awali wakati kuna mtu ana ushahidi wa kuthibitisha namna fedha chafu zinavyoingia nchini.

“Sitaki kuamini kama IGP ana maslahi katika hili lakini pia sisiti kuamini kuwa hii si kauli ya Nape ni ya kiongozi wake mkuu katika Chama, sasa kwa hili wanazidi kutudhihirishia kuwa nchi imewashinda kwa kuwa kuna vyombo vya usalama vinavyoongozwa na serikali ya   CCM vimeshindwa kuchukua hatua na kuudhihirishia umma ukweli unaosemwa na Nape”alisema Dk Slaa.

Mwananchi

Posted by Editor on 14:28. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for Serikali yaingilia kati mgogoro wa Chadema, CCM

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery