WABUNGE CCM WAOMBA KUSAFISHWA NA PINDA
TUHUMA za rushwa dhidi ya wabunge juzi zilitawala kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM, ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliombwa kuingilia kati ili ‘kuwasafisha’ wenye tuhuma hizo mbele ya jamii. Kikao hicho kiliitishwa pamoja na mambo mengine, kuzungumzia nafasi ya wabunge wa CCM katika kuhamasisha umma kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 26, mwaka huu na utoaji wa maoni kwa Tume ya Katiba Mpya.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zimesema pamoja na kwamba haikuwa moja ya agenda za mkutano huo, Mbunge wa Bukene, Seleman Zedi alisimama na kuibua kilio cha wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa. Mbunge huyo ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda alimweleza Waziri Mkuu kwamba baadhi ya wabunge, hasa wa iliyokuwa kamati yake, wangekwendaje kuhamasisha Sensa majimboni wakati wamechafuka kwa tuhuma za rushwa?
Mtoa taarifa wetu anasema, mbunge huyo akiungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe, walimwomba Waziri Mkuu ambaye ni mwenyekiti
wa kikao hicho, amweleze Spika awasafishe kwa kutangaza bungeni kwa madai kuwa tuhuma dhidi yao hazikuthibitika.
Alisema kauli hiyo ya Spika ingewasaidia kurudi majimboni wakiwa wasafi na wenye mamlaka ya kimaadili kuungana na wenzao kuhamasisha Sensa na utoaji wa maoni ya Katiba Mpya. Hata hivyo, vyanzo vyetu vya habari vimetofautiana kuhusu kauli ya Pinda baada ya kupokea malalamiko hayo, kimoja kikisema alikaa kimya na kingine kikisema alijibu kuwa asingeweza kuingilia kati suala hilo kwa kuwa bado linachunguzwa na Kamati ndogo ya Bunge. Mambo mengine yaliyoibuka kwenye kikao hicho ni mjadala wa Muswada wa Fedha.
Wabunge wa CCM walipinga ongezeko la kodi kwenye maji ya kunywa na msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwa kampuni za kuchimba madini. Kwa zaidi ya wiki sasa, Kamati ndogo ya Bunge iliyoundwa na Spika Makinda imekuwa inaendelea kuwahoji baadhi ya wabunge ama wanaotuhumiwa au wenye ushahidi wa tuhuma hizo. Baadhi ya wabunge wamekuwa wakiitwa mmoja baada ya mwingine na kuhojiwa na wajumbe hao faragha kuhusu ama madai ya rushwa dhidi yao au mambo waliyoeleza kuhusu tuhuma hizo. Tuhuma hizo zilisababisha Spika Makinda kuvunja Kamati ya Nishati na Madini iliyodaiwa kukithiri kwa rushwa.
Kamati inayoendesha uchunguzi huo inaongozwa na Mbunge wa Mlalo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Hassan Ngwilizi. Wajumbe wake ni John Chiligati
(Manyoni Magharibi), Riziki Omar Juma (Viti maalumu), Said Amour Arfi (Mpanda Mjini) na Gosbert Blandes (Karagwe). Hadi sasa wabunge kadhaa wanatajwa kuwa wamekwishahojiwa, akiwamo Anna Kilango Malecela (Same Mashariki-CCM), ambaye hata hivyo, alipoulizwa
aling’aka akisema mambo ya kamati ya maadili ni siri hayaruhusiwi kusemwa popote. Wengine wanaotajwa ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Vicky Kamata, (Viti Maalumu (CCM), Sara Msafiri (Viti Maalumu, CCM) na Tundu Lissu (Chadema). Wengine ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi. Wabunge wengine walioitwa kuhojiwa akiwamo Ally Keisy (Nkasi), John Mnyika (Ubungo), Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) na wengine, hadi jana iliyokuwa siku ya mwisho, walikuwa hawajakutana na kamati hiyo.
Tume hiyo ilipewa wiki mbili ambazo zilikuwa zinamalizika jana. Naibu Spika, Job Ndugai alipoulizwa iwapo kamati hiyo imeongezewa muda aliomba apewe muda kwa kuwa alikuwa anaingia kwenye kikao kitakachojadili suala hilo. “Naingia kwenye kikao sasa, tunazungumzia suala hilo, ukinitafuta baada ya saa moja nitakuwa na jibu la kukupa,” alisema. Baadaye alisema: “Kikao hicho kilikuwa na mambo mengi na Ngwilizi hakupata fursa ya kusema chochote kuhusu kamati yake. Ila Spika angetoa mwongozo kabla hajaahirisha Bunge.”
Tuhuma za wabunge
Tuhuma hizo ziliibuka wakati wa kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2012/13. Baadhi ya wabunge walidai kuwa kuna wenzao wamehongwa na kampuni za mafuta ili kushinikiza Waziri Muhongo na Maswi wang’olewe katika nafasi zao kwa kukiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma.
Shinikizo hilo linadaiwa kuwa lilitokana na wizara hiyo kuipa zabuni kampuni ya Puma Energy kwa ajili ya kuiuzia Serikali mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura ya IPTL na kuachwa kampuni binafsi, uamuzi ulioelezwa kuokoa fedha za walipa kodi Sh72 bilioni kwa mwaka.
Baada ya kutolewa madai hayo, Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM), alitoa hoja akitaka kuvunjwa kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kutokana na wajumbe wake kutuhumiwa kuhongwa na hoja ikakubaliwa na Spika Makinda akaivunja na kuunda kamati hiyo ya Ngwilizi.
Hadidu za rejea za kamati hiyo ni kuchunguza tuhuma kama baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini walijihusisha na vitendo vya rushwa au la.
Alisema kamati hiyo imeundwa kwa mujibu wa Kanuni ya 114 (18) kwa lengo la kuwezesha uchunguzi kufanyika haraka.
Kamati hiyo inatakiwa kupitia kumbukumbu rasmi za Bunge za Julai 27 na 28, mwaka huu na Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliwasilishwa ili kupata picha ya namna mjadala mzima ulivyoendeshwa, kisha kuwaita na kuwahoji mashahidi ambao wataisaidia kamati kujua ukweli wa tuhuma hizo.
Lissu, ambaye ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika mkutano wake na waandishi wa habari, alitaja majina ya wabunge kadhaa wenye mgongano wa kimasilahi na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Alitajwa kuwa shahidi muhimu miongoni mwa wanaopaswa kuhojiwa.
Posted by Editor
on 10:58.
Filed under
eastafricannews
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0