Yanga Yarejea Nchini Bila Beki Mbuyu Twite
Baadhi
ya wachezaji wa timu ya Yanga wakiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana wakitokea katika
ziara ya michezo ya kirafiki nchini Rwanda
--
MASHABIKI wa soka nchini wameendelea kutoamini macho yao,
baada ya Mabingwa wa Soka Afrika Mashariki na Kati Yanga jana kutua
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere jijini Dar es Salaam
ikitokea Kigali, Rwanda, bila ya beki wake mpya aliyecheza mechi za kirafiki nchini humo Mbuyu Twite.
Twite aliyesajiliwa na Yanga akiwa Rwanda
na kisha kubaki huko hadi alipoungana na timu nchini humo na kucheza
mechi hizo za kirafiki, alitarajiwa kutua jijini na Wanajangwani hao,
ambapo mashabiki wa Yanga na wa Simba walisubiri ujio wake.
Kusubiriwa kwa
hamu kwa Twite kunatokana na mkanganyiko aliozua katika usajili wake,
ambapo awali alisajiliwa na kutambulishwa na Simba akitokea APR ya Rwanda alikokuwa akicheza kwa mkopo, kabla ya Yanga kutibua dili hilo na kumsainisha kupitia klabu yake ya zamani ya Lupopo ya DRC.
Licha ya kutowasilisha jina lake kwa
TFF, Simba imeendelea kulia na Twite iliyemtangaza kuwa tapeli na
kumfungulia jalada (RB) la wizi wa kuaminika wa dola za Kimarekani
30,000 za usajili, huku ikimtaka kurejesha fedha hizo mwenyewe kama alivyopewa.
Akizungumza na
waandishi wa habari uwanjani hapo wakati msafara wa watu zaidi ya 40
Yanga, wakiwamo wachezaji 28 ulipopokelewa, Katibu Mkuu wa Yanga
Mwesigwa Celestine, alisema kuwa, Twite atawasili nchini wakati wowote
na kuwa amebaki Kigali akikamilisha baadhi ya mambo.
“Hakuna cha
kumtish Twite kiasi cha kutoungana nasi kuja Dar, kuna taratibu muhimu
anashugulikia. Atatua nchi wakati wowote na tutakuwa naye katika pambano
letu na Coastal Union hapo Jumamosi,” alisema Mwesigwa akikana habari zilizozagaa uwanjani hapo kuwa alihofia kutiwa mikononi na Simba.