TAMKO LA TEF KUHUSU UONGOZI WA WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO KUTOSHIRIKI MKUTANO WA WAHARIRI NA MCT MKOANI MOROGORO
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda
UTANGULIZI
Juni 3 – 5, 2012, wahariri watendaji na waandamizi wa vyombo vya habari nchini walikutana mjini Morogoro katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Mashauriano kati yao na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Mkutano huu ulioshirikisha wahariri kutoka katika vyombo vya serikali, binafsi na vile vinavyomilikiwa na vyama au taasisi za kidini pamoja na mambo mengine ulijadili hali na mwenendo wa vyombo vya habari hapa nchini kwa sasa na kwa siku zijazo.
Katika mkutano huo zilijadiliwa mada mbalimbali ambazo kwa ujumla wake zililenga kuwezesha kazi ya uandishi wa habari kufanyika kwa kuzingatia maadili, wajibu na weledi wa kitaaluma.
Pia mada hizo zililenga kuimarisha, weledi wa kitaaluma, uwajibikaji utendaji wa kazi, na uhuru wa vyombo vya habari na zaidi kujenga mfumo wa usimamizi wa maadili ndani ya vyombo vya habari.
Mbali ya hayo, wahariri na wadau wengine wa habari waliohudhuria mkutano huo walijadili kuhusu Mchakato wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari na Huduma za Vyombo vya Habari nchini ambao umekuwa ukisuasua kwa takriban miaka 10 sasa.
Ifahamike kwamba, mkutano huu ulikuwa na uzito wa pekee hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba, wahariri ndio wasimamizi na watoa uamuzi wa mwisho katika vyumba vya habari kuhusu masuala yote yanayohusu habari, makala na taarifa zinazotolewa katika vyombo wanavyofanyia kazi.
USHIRIKI WA SERIKALI
Kwa masikitiko makubwa, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Seth Kamuhanda hawakushiriki hata kwa kufungua mkutano huu kama walivyoombwa na Baraza la Habari Tanzania na wao wenyewe kuthibitisha kwa nyakati tofauti.
Kwa mshangao wa wahariri na wadau wengine waliohudhuria mkutano huo, viongozi hao wawili mbali ya kutumiwa rasimu ya hotuba ambayo ilipaswa kusomwa kwanza na waziri ambaye ndiye alipaswa kuwa mgeni rasmi, kabla ya yeye mwenyewe (waziri) kutoa taarifa MCT kwamba, angewasilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hawakutokea katika mkutano huo wala kutuma mwakilishi mwingine yoyote, huku wakitoa udhuru kwamba walikuwa na kazi nyingine.
Hatua ya viongozi hao kushindwa kufika katika mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya tasnia ya habari nchini ikiwa ni pamoja na kushindwa kwao kutuma mwakilishi mwingine kutoka wizarani, si tu iliwashtua wahariri, bali iliwasononesha na kuwashangaza.
Taarifa ambazo tulizipata zinaonyesha kuwapo kwa msuguano usio na afya kwa tasnia ya habari, kwa wizara na kwa serikali nzima kati ya Waziri na Katibu Mkuu. Kitendo cha wao kushindwa kutuma mwakilishi kutoka kwa viongozi na watendaji wengi waliojaa katika wizara hiyo ni ushahidi wa namna hali ilivyo mbaya na tete kimahusiano na kikazi katika wizara hiyo.
MTIZAMO WA WAHARIRI
Kitendo cha wiki hii kinatupa mashaka iwapo tunastahili kuendelea kuwa na uongozi wa Waziri na Katibu Mkuu wa sasa katika wizara hii. Tunasema hivyo kwani tuna shaka sana kama siku zijazo watatoa ushirikiano wa kutosha, hasa katika mchakato wa kupata sheria nzuri za Huduma za Vyombo vya Habari na ya Haki ya Kupata Habari.
Tukio hili kwetu wahariri limetupunguzia imani kwa viongozi hawa iwapo wataweza kutuvusha katika mabadiliko ya kitaaluma na yale ya kimfumo katika kukusanya na kutoa habari nchini.
Kwa maana hiyo tumeazimia kwamba kwanza; Tunatoa taarifa rasmi ili umma wa Watazania uweze kufahamu hali hii, lakini pili tutawasilisha rasmi malalamiko yetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aweze kuingilia kati hali hii kwa nia ya kuiokoa tasnia ya habari, ambayo ni muhimu kwa ustawi na afya ya taifa hili.
Tunapenda kuwahakikishia Watanzania na Serikali kwa ujumla kuwa vyombo vya habari vimejizatiti na kujipanga kuwatumikia Watanzania kwa kuzingatia maadili na weledi wa hali ya juu pia kwa kuzingatia matakwa na maslahi ya umma.
Tunachoomba ni zana za kufanyia kazi hii. Zana hizi si nyingine bali ni Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na Sheria ya Haki ya Kupata Habari, ambazo mchakato wake umedumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa bila sheria hizi kupatikana.
Tunasema mikingamo inayokwamisha sheria hii imalizwe ili tuweze kupata sheria nzuri na kufanya kazi kwa uhuru na uhakika zaidi.
Hili la Waziri na Katibu Mkuu wizarani linaongeza wasiwasi wa kupatikana kwa sheria hizi.
Mungu ibariki Tanzania.
Neville Meena,
Katibu – Jukwaa la Wahariri (TEF)
Dar es Salaam,
Juni 07, 2012.




