Share this Post

dailyvideo

Tanzania Ni Zaidi Ya Uijuavyo!



Ndugu zangu, 


Huko nyuma nilidhani barabara ya kutoka Arusha kupitia Old Monduli Road, Simanjiro hadi Dodoma ni ngumu sana. Hapana, jana nilifuata ramani ya satelite ya google. 


Nilitoka Makambako, nikapanga kuikuta Madibira, Mbeya kupitia Malangali, Iringa. Aisee, haikuwa shughuli ndogo. Nilipofika kijiji kinaitwa Kwatwanga nikaikuta barabara inayokwenda Kwale hadi Saadani. Na hapo kuna njia ya mkato kwenda Madibira kukatisha pori lililoshona. 

Ni njia ya watembea kwa miguu na baiskeli. Ni umbali wa kilomita 40 hivi kabla ya kufika kijiji cha Mapogolo iliko barabara ya kutoka Rujewa kwenda Madibira.  Sijapata kuiona njia nyembamba kama ile. Sehemu nyingine ilikuwa na mashimo kiasi unalazimika kupasua njia nyingine. Sehemu nyingine ilikuwa na mchanga mwingi. Na njia nzima hakuna mtandao wa kampuni yeyote ya simu. Hakukuwa na mawasiliano.

Njiani nilikutana na baiskeli moja tu na watembea kwa miguu watatu wakiwa na mizigo. Vinginevyo pori limetulia na linatisha. Kuna visiki vingi na unakwenda kwa kuvitafuta vichochoro vya porini.

Ilinichukua saa nzima na nusu nikiwa porini. Kuna mahali nilisimama kukata matawi ya miti ili nipite. Hapo kukawa na mbung'o wengi. Bahati nilikuwa na mtani wangu kijana wa Kinyamwezi aliyenisindikiza kutoka Iringa, anaitwa  Isike Maganga. Tulishuka na kusafisha njia kwa haraka na kuondoka mahali hapo. 

Tulipofika Mapogolo nilijisikia kuchoka sana. Nikajawa na fikra nyingi sana kuhusu miundo mbinu yetu. Nilijiona mjinga pia kwa kuamini ramani ya satelite ambayo ilinionyesha kuwa kuna njia pana kutoka Kwatanga kwenda Mapogolo.

 Fikiri Kifaru changu kingeniharibikia porini, nilikuwa sina msaada wowote bali  kuchagua; ama kutembea kwa miguu hadi Mapogolo, au kupiga kambi porini kwa maana ya kukesha usiku kucha. Ndio maana porini kuna umuhimu wa kutembea na kibiriti, tochi, chepeo na hata panga la kukatia matawi ya miti, zaweza kuwa kuni za kukufanya uishi.

Hakika, Tanzania ni zaidi ya uijuavyo!
Maggid,
Iringa.

Posted by Editor on 14:59. Filed under , , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for Tanzania Ni Zaidi Ya Uijuavyo!

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery