Share this Post

dailyvideo

Warioba awapiga 'stop' RC, DC

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amewapiga marufuku viongozi wa serikali kuhudhuria katika mikutano ya wananchi ya kukusanya maoni ya katiba.

Jaji Warioba alitangaza zuio hilo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari, alipotembelewa ofisini kwake na viongozi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), jijini Dar es Salaam jana.

Alisema maoni yanayokusanywa awamu hii ni ya wananchi, na kwamba ni vyema kuwaachia wakatoa maoni yao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu.
“Mchakato huu ni shirikishi, kila mtu atapata nafasi ya kutoa maoni yake, tukimaliza kwa wananchi tutakuja katika kada nyingine, hivyo hakuna haja ya kuwaingilia wananchi, waachwe watoe maoni yao wenyewe,” alisema na kuongeza:
“Tukimaliza kwa wananchi tutakuja katika kada nyingine, kama vile wanaharakati, walimu, wakulima na nyingine zote.”
Aliotakiwa kufafanua viongozi hao ni kama kina nani alisema ni wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa kwa kuwa kama watakuwa kwenye mikutano ya wananchi, kuna uwezekano wa wananchi kutokuwa huru kutoa maoni yao kwa sababu viongozi hao kuwako.
"Mwananchi wa kawaida ambaye anakwenda kutoa maoni yake ya Katiba mpya kama akimkuta kiongozi wake kama Mkuu wa Mkoa au Wilaya ataogopa kusema," alisema.
Alisema kuwa wananchi wanawaheshimu viongozi wao, kwa hiyo uwepo wao katika mikutano yao unaweza kukwaza uhuru wa utoaji wa maoni.
Alisema jumla ya watu 27,000 walipata nafasi ya kutoa maoni yao katika awamu ya kwanza, na kwamba zoezi la ukusanyaji wa maoni kwa upande wa wananchi linatarajiwa kumalizika Novemba mwaka huu.
Aliongeza kwamba katika zoezi la ukusanyaji wa maoni, hakuna uchakachuaji wala kutishiwa kama inavyodaiwa, kwa sababu kila mtu anapewa nafasi ya kutoa maoni yake.
“Hatutaki dalili zozote ambazo zitakuwa zinaonyesha kutishia wananchi  kutoa maoni yao, wala sisi hatuwatishii, isipokuwa nia yetu ni kuwafanya wananchi wawe huru kutoa maoni,” alisema na kuongeza:
“Tunakubali maoni yoyote yanayohusiana na katiba, hata yale yanayotolewa katika mitandao au yanayotolewa kupitia vyombo vya habari yote tunayakusanya.”
Alisema katika awamu hiyo wanatarajia kuongeza idadi kubwa zaidi ya wananchi katika mchakato huo wa kupata maoni ya katiba.
CHANZO: NIPASHE

Posted by Editor on 14:17. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for Warioba awapiga 'stop' RC, DC

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery