Mchungaji Msigwa: Waliofukuzwa Maliasili ni dagaa
Siku moja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kuwafukuza kazi watumishi watatu wa idara ya Wanyamapori, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) amesema waliofukuzwa kazi kwa kosa la utoroshaji wanyamapori ni dagaa kwa kuwa wanamtandao waliopendekezwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu na Kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyochunguza sakata hilo, wameachwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo iliyosomwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, Aprili 29, mwaka huu ambayo NIPASHE imeiona, inapendekeza aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dk. Erasmus Tarimo, achukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa mwaka 2009, Dk. Tarimo aliingia mkataba na raia mmoja wa Pakistan, Kamrani Ahmed, uliowezesha kutoroshwa tembo wanne wakiwa hai kwenda nje ya nchi.
Inaeleza kuwa Kamrani ana kesi nyingi za ukamataji na usafirishaji wa wanyamapori hai kinyume cha sheria na pia anamiliki kadi ya ukamataji wanyama hai namba 0016929 ilhali ni raia wa kigeni ambaye haruhusiwi kuwa na kibali hicho.
Kamrani anadaiwa kuingia mkataba huo kama mwakilishi wa serikali ya Pakistan, wakati yeye ni mfanyabiashara wa uwindaji wa kitalii kupitia kampuni ya Jungle International.
Kamati hiyo ilibaini kuwa kampuni ya Jungle imepewa kibali cha kukakamta wanyama hao kufanyika katika wilaya tatu za Longido, Simanjiro na Monduli, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni kwani kibali cha kukamata wanyama ni lazima kiainishe wilaya moja tu.
Hata hivyo, kanuni inataka kama kuna ulazima wa kukamata wanyama katika wilaya zaidi ya moja basi vitolewe vibali tofauti kwa kila wilaya.
Kamati hiyo ndogo ilibaini kuwa Machi 23, 2009, Idara ya Wanyamapori ilimuandikia mkurugenzi mtendaji wa jiji la Karachi barua yenye kumbukumbu namba GD/R40/20/Vol11/8 kumuarifu kwamba maombi yake ya kukamata tembo majike wanne yamekubaliwa, lakini hapakuwa na uthibitisho wa Serikali ya Karachi kupokea tembo hao.
Pia iliilaumu wizara kwa kushindwa kuiletea kamati nyaraka kwa wakati kiasi kwamba baadhi ya mazingira ilibidi kutumia vyombo vya dola kufuatilia nyaraka hizo.
“Kwa mfano, nyaraka ambazo kamati iliagiza iletewe kutoka CITES-Arusha na Kikosi cha Kuzuaia Ujangili-Arusha kutoka Desemba, mwaka jana hadi leo (siku ilipowasilishwa ripoti), hazijawasilishwa kwenye kamati,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo yenye kurasa 95.
Aidha, Kamati ilipendekeza wote waliohusika na kutoa kibali hicho wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Msigwa ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, alisema watendaji hao wametolewa kama kafara kwa kuwa wapo watendaji ambao walipendekezwa kuchukuliwa hatua na kamati hiyo ndogo, lakini hadi leo bado hawajachukuliwa hatua.
“Ujangili ni mtandao mkubwa siyo kwa kuwafukuza kazi hao ndiyo amemaliza tatizo la ujangili. Wapo watu ambao kamati yetu ndogo iliwataja bungeni hawajachukuliwa hatua,” alisema .
Msigwa alisema waziri kuwafukuza kazi watumishi watatu ni kuwahadaa wananchi kwa kuwa amewaacha wale mafisadi waliobobea ambao wako katika nyadhifa za juu walioongoza mchakato mzima wa kusafirisha twiga kwenda nje.
“Hivi inawezekanaje ndege ya Jeshi la Taifa lingine iingie nchini na kubeba wanyamapori kwenda nje, ratiba ya ndege zinazowasili nchini isionyeshe hivyo au hata rada za jeshi letu zisiione? Hii inaonekana kwamba kuna mtandao mkubwa wa ujangili wa kimataifa ambao serikali inaujua na inashirikiana nao,” alisema na kuongeza:
“Pia waziri asijisifu kwa kwa kuwafukuza watumishi watatu na kutoa onyo kwa wengine kwani hata waziri aliyemtangulia alifanya hivyo hivyo. Pia Waziri Kagasheki akumbuke wosia wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwamba serikali inayokimbizana na watu wadogowadogo ni serikali dhaifu na ni Serikali ‘Corrupt.’”
Kadhalika, Msigwa alisema Balozi Kagasheki hakujibu hoja za msingi katika hotuba ya Kambi ya Upinzani wakati wa bajeti ya wizara yake, na badala yake aliamua kuujadili uchungaji wake.
Pia alilalamikia kitendo cha waziri kutumia muda mrefu kufanya propaganda kuhusu kosa la uchapaji la jina la kiongozi wa CCM, (jina tunasitiri), ambaye anatuhumiwa kwa ujangili wilayani Karatu badala ya kushirikiana na Kambi ya Upinzani katika kuwasaka na kuwatokomeza majangili wa maliasili za taifa.
Kuhusu maazimio na mapendekezo ya kamati ndogo ya Bunge ya
SERIKALI YASHAURIWA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI
Katika hatua nyingine, serikali imeshauriwa kuwafikisha mahakamani vigogo wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii wanaotuhumiwa kuhusika kwenye kashfa ya kusafirisha nje wanyama hai 136, pamoja na ndege 16, wenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 100.
BANA: WASHITAKIWE
Akizungumza na NIPASHE jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema halitakuwa jambo la busara kwa watuhumiwa hao kuishia kufukuzwa au kusimamishwa kazi tu, bali washtakiwe kwa kulisababishia taifa hasara kubwa.
“Endapo kutakuwa na ushahidi ni vyema wakashtakiwa kwa kulisababishia taifa hasara kubwa kuliko kuwaachia wakipita mitaani kwa furaha,” alisema Dk. Bana.
KIMARO: HATUA ZAIDI
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, Idara ya Elimu ya Binadamu, Asili, Maendeleo na Utalii, Frank Kimaro, alisema endapo wizara imefanya utafiti na kuridhika kuwa watendaji hao wana makosa ni vyema wakachukuliwa hatua zaidi ya kufukuzwa, lakini kama hatua hiyo ni danganya toto, basi bado kuna kazi kubwa.
Kimaro aliongeza kuwa kitendo cha kuwawajibisha watendaji wa wizara hiyo, kama siyo kuwatoa kafara kama ilivyozoeleka, basi ni mwanzo mzuri kwa waziri huyo na amemtaka kuufumua na kuuteketeza mtandao wa hujuma za rasilimali za nchi ambao umekuwapo miaka nenda rudi.
BAREGU: MWAZO MZURI
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Saint Augustine, Mwanza, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Profesa Mwesiga Baregu, alisema wizara hiyo ni moja kati ya wizara zenye matatizo sugu na ya muda mrefu na kusema kitendo cha waziri kimeonyesha kuwa ana lengo la kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo.
Profesa Baregu alisema ni lazima kuwepo kwa vikwazo mbalimbali, kwani siyo watu wote wanaopendezwa na hatua kama hiyo kwa kuwa kuna kuyagusa maslahi binafsi.
Alimtaka waziri huyo asimwangalie mtu usoni kwenye kutoa maamuzi magumu kama hayo.
Aidha, alimtaka Kagasheki kuwa na mkakati imara na wa muda mrefu ili kuhakikisha anauondoa uozo wote uliopo kwenye wizara hiyo, pamoja na kuwa na mbinu, na kubadili taratibu zote zisizofaa, na kubadili baadhi ya sheria zenye upungufu.
TANAPA: HATUNA HAKIKA
Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), imesema haina uhakika iwapo meno ya tembo yanayokamatwa nchi mbalimbali duniani, asilimia 42 yanatoka nchini.
Pamoja na ujangili wa kuua tembo, ujangili mwingine unaotisha upo kwa mauaji ya faru ambao ni moja ya wanyama walio kwenye hatari kubwa ya kutoweka duniani.
Akizungumzia ujangili dhidi ya tembo, Meneja Uhusiano wa Tanapa, Paschal Shelutete, alisema jijini hapa wakati NIPASHE ilipotaka kupata maoni ya Mamlaka hiyo kuhusu madai hayo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema juzi aliwaeleza wanahabari jijini hapa kuwa hali ya ujangili kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba nchini ni mbaya.
Alisema taarifa zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 1989 – 2010 robo ya meno ya tembo yaliyokamatwa duniani kote yanatoka Tanzania.
“Sina uhakika kama asilimia 42 ya meno hayo yanatoka kwetu, Hata hivyo, ujangili wa meno ya tembo ni mkubwa siku hizi kwa sababu unachangiwa na mitandao ya ujangaili ya kimataifa,” alisema Shelutete.
Mwaka juzi, Tanzania ilizuiwa na Shirika la Kimataifa linalojihusisha na kulinda wanyama walio katika hatari ya kutoweka duniani, (CITES), kuuza tani 80 za meno ya tembo zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 20 kwa kile kilichoelezwa kwamba kufanya hivyo kutachochea vitendo vya ujandili wa wanyama hao. Pia Tanzania ililaumiwa kwa kutokufanya juhudi ya kutosha kuteketeza ujangili mbugani.
Na katika hatua nyingine, Katibu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, ameilipua tena serikali kwa kutumia nyaraka za siri, akisema kuwa anazo taarifa kuhusu mauaji ya faru yaliyofanyika hivi karibuni.
Dk. Slaa amedai kuwa kuna mtandao mkubwa wa ujangili unaohusisha watu wakubwa serikalini, watumishi wa vyombo vya dola, wakiwemo askari polisi na watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Dk. Slaa alisema mauaji ya wanyama adimu kama faru yaliyofanyika hivi karibuni katika Mbunga ya Serengeti, ni dalili ya hujuma kubwa katika sekta ya maliasili ambazo zinafanywa na mtandao huo, huku akilitaka Bunge kuacha kunyamazisha wabunge wanaotaka kupanua mjadala wa ufisadi mkubwa unaoendelea kuteketeza maliasili za nchi, wakiwemo wanyama kama twiga na faru.
Pia alisema inashangaza kuona serikali imeendelea kufumbia macho mtandao huo wa ujangili unaohusisha watu walioko serikalini hivyo kuendelea kukuza tatizo la ufisadi wa rasilimali za nchi.
Akiwahutubia mamia ya wananchi katika vijiji vya Kata ya Malinyi, Mikumi na Ruaha, alisema anazo taarifa za siri, kutokana na barua za viongozi na watendaji serikalini zinazoelezea kwa upana suala zima la mtandao wa ujangili, ambazo pia zinaelezea kwa undani tukio la kuuawa kwa faru hao wawili huko Serengeti.
Alisema inashangza mpaka sasa hakuna hatua za haraka zimechukuliwa kushughulikia kiini cha tatizo hasa kwa kuanzia na mtandao huo.
Akiwa katika Kata ya Malinyi na Mikumi juzi, Dk. Slaa alisema ni ajabu kubwa katika nchi inayotaka kuendelea watumishi wa idara nyeti badala ya kujishughulisha na usalama wa kiuchumi (economic intelligence) wanahangaika kufuatilia wakosoaji wa chama kilichoko madarakani.
Alitolea mfano ambavyo Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi nchini wamekuwa wakifuatilia nyendo za Chadema na viongozi wake.
“Kwa wale wanaofuatilia Bunge, watakuwa wameona juzi Mbunge wa chama chenu Chadema wa Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa, alivyoambiwa bungeni baada ya kuibua suala hili la kuuawa kwa faru…mimi sitaki kuingia huko kwenye kamati yao na kile wanachofanya, lakini documents (nyaraka) nilizonazo hapa zinaeleza bayana namna ambavyo faru hao waliuawa huku wahusika wanaotajwa wakiwemo askari polisi na majina wametajwa hapa.
Maliasili zetu wakiwemo wanyama, ziko hatarini kumalizwa kutokana na uzembe wa serikali kulea ufisadi,” alisema.
Aliongeza: “Kosa la Msigwa kama ambavyo akina Lukuvi wanataka kuonyesha ni kumtaja mmoja wa viongozi wa CCM kuwa anahusika katika mtandao huu wa ujangili, lakini hilo siyo suala, kwa sababu taarifa zilizopo zinamtaja huyo kiongozi wa CCM kutoka Karatu, kinachoonekana kukosewa hapa ni kwamba taarifa zinamtaja bwana huyo kuwa ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Karatu, Lukuvi anasema aah, hakuna kiongozi wa CCM Wilaya ya Karatu mwenye jina hilo, lakini tumechunguza na kubaini kuwa huyo aliyetajwa ni mwenyekiti wa kijiji anayetokana na CCM huko huko Karatu.”
Jana akiwa katika maeneo mbalimbali ya vijiji vya Mikumi, ikiwemo Ruaha, Dkt. Slaa alisema anashangazwa na kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki kusema kuwa kama maamuzi yangelikuwa ni ya kwake angechukua maamuzi makubwa zaidi juu ya matatizo yanayoikabili wizara yake, hususan sekta ya uwindaji na wanyama pori, akihoji kwa nini waziri huyo bado yuko kazini kama anaona kuna watu wanamkwaza kufanya maamuzi.
“Hiyo ndiyo maana ya kuwajibika. Kama Kagasheki anaona kuna mahali angeweza kuchukua hatua lakini anashindwa kwa sababu kuna watu wengine wanapaswa kuchukua hatua lakini hawachukui hatua basi aondoke. Na sisi wengine tunaelewa anaposema hivyo, kwa sababu ninayo hapa barua yake akimtaarifu Waziri Mkuu Pinda juu ya tukio la kuuawa kwa faru lakini mpaka sasa hakuna hatua.
“Katibu Mkuu wa wizara hiyo katoa taarifa, hakuna hatua. Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA katoa taarifa ya kina hakuna hatua mpaka sasa, wameunda kikosi cha uchunguzi kimetoa taarifa ya kina, hakuna hatua zozote mpaka sasa, hivyo tunaelewa anaposema maamuzi yangekuwa ya kwake, lakini kama wakubwa wake wanamkwaza ajiuzulu. Maana hii ndiyo serikali ya CCM na akina Kikwete, pale ambapo maslahi ya wakubwa serikalini, kwenye CCM yao na mitandao ya ufisadi, yanaguswa maamuzi hayachukuliwi.
Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA alisema anayo barua kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki kwenda kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ikielezea namna ambavyo faru hao waliuawa, lakini pamoja na wahusika kutajwa, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao, kutokana na mtandao huo wa ujangili kuhusisha watu wakubwa, askari na watu wa Usalama wa Taifa.
Kutokana na kutoshughulikia kiini cha matatizo katika Wizara ya Maliasili na Utalii, amesema kamwe Waziri Kagasheki asifikiri amemaliza tatizo kwa kufukuza watu na kuwashusha vyeo.
Imeandaliwa na Sharon Sauwa na Restuta James, Dodoma; Samson Fridolin, Dar na John Ngunge, Arusha.
CHANZO: NIPASHE
Posted by Editor
on 14:14.
Filed under
eastafricannews
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0