CWT yalikataa Baraza la Majadiliano
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeingia katika mvutano mwingine na Serikali baada ya kutangaza kulikataa Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Walimu lililoundwa kwa mara ya pili na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Baraza hilo lililozinduliwa juzi na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mulugo, limekataliwa na CWT kwa madai kuwa halina uwezo wa kusuluhisha migogoro kati ya walimu na Serikali.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba (pichani), akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema baraza lililoundwa na wizara halina mamlaka ya kutatua migogoro sehemu ya kazi kama iliyokwishajitokeza baina ya watumishi na serikali.
“Kazi ya Baraza hili ni kuishauri serikali kuhusu njia mbalimbali za kuzuia kutokea kwa mgogoro, chombo pekee chenye mamlaka ya kushughulikia migogoro ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambako CWT ilipeleka mgogoro wake na kufikia hatua ya kutoelewana,” alisema Mukoba.
Mukoba alisema CWT kinatambua kuwa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja kwenye Utumishi wa Umma inazuia mabaraza ya majadiliano ya kisekta kufungua upya majadiliano baada ya majadiliano kuhitimishwa na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali hadi ipite miezi 12.
Alisema kutokana na mgogoro uliopokati ya walimu na serikali ya kutaka maslahi bora, baada ya suala hilo kuamuriwa na mahakama, walimu wamerudi kazini wakiwa wamekosa ari ya kufanya kazi kutokana na mwajiri wao kuwapuuza.
“Serikali wasitufanye kama nyani kwa kutuning’izia mahindi mabichi yaliyojaa moshi na ikiwa wanafahamu hatuwezi kuyala,” alisema Mukoba na kuongeza kuwa kimsingi walimu hawatafanya kazi kwa moyo hadi majadiliano yatakapofanyika mwaka ujao wa fedha.
Alisema ili kufikia mwafaka mgogoro uliopo, serikali iteue timu ya watu wachache kutoka serikalini kwa ajili ya kujadiliana na viongozi wa CWT nje ya Baraza la Majadiliano ya Pamoja kwenye Utumishi wa Walimu kama ilivyofanyika kwa madaktari.
“Wakati wa mgogoro wa madktari, Waziri Mkuu aliunda timu ya watu wachache waliojadili mgogoro uliokuwepo kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, mbona madaktari hawakulazimishwa kujadili madai yao kwenye Baraza la Majadiliano ya Pamoja kwenye sekta ya afya ambayo ipo kisheria?” alihoji Mukoba.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mulugo, akizindua Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Walimu, aliliagiza lianze majadiliano ya kutatua mgogoro kati ya walimu na serikali mara moja.
habari na THOBIAS MWANAKATWE
chanzo NIPASHE




