John Mnyika:Ujenzi wa Barabara ya maziwa-External kwa kiwango cha lami waanza

Mbunge wa jimbo la Ubungo(CHADEMA)Mh John Mnyika
---
Tayari
taratibu za zabuni zimeshakamilika na mkandarasi anapaswa kuanza
ujenzi. Manispaa ya Kinondoni imeshaweka alama ya "X" katika majengo
ambayo yatapaswa kubomolewa kuwezesha upanuzi wa barabara husika
unaofanywa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es salaam (TANROADS).
Tarehe
15 Septemba 2012 nilifanya mkutano wa hadhara Jimboni Ubungo kwenye
kata ya Makuburi ambapo pamoja na maswali mengine niliulizwa ni lini
ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami kutoka Maziwa mpaka External
ukiambatana na ujenzi wa daraja katika barabara husika utaanza.
Pamoja
na kueleza hatua iliyofikiwa mpaka sasa nilitoa mwito wananchi wote
ambayo makazi yao yamewekewa alama ya "X" ikiwa si wavamizi wa barabara
wawasilishe kwa Manispaa ya Kinondoni maelezo na vielelezo vyao kwa
kuzingatia Wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es es salaam (TANROADS) wao
wana bajeti ya ujenzi pekee na madai ya fidia kwa wenye uhalali yako
chini ya Manispaa ya Kinondoni; tayari 17 Septemba 2012 baadhi ya
wananchi wamewasilisha nyaraka zao.
Ikumbukwe pia
kuwa kwa kutambua umuhimu wa suala hili nilichukua hatua mbalimbali za
kibunge kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2011 ili barabara husika iweze
kupandishwa hadhi na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa haraka zaidi
kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kuliko ilivyopangwa awali.
Niliziandikia
mamlaka husika hususan Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuzingatia barabara
tajwa katika bajeti kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano,
Wizara ya Ujenzi awali ilisema serikali kuu haiwezi kushughulikia
barabara hiyo kwa kuwa iko chini ya Manispaa ya Kinondoni. Lakini,
nikaendelea kuchukua hatua zaidi kwa njia za kibunge na za uwakilishi wa
wananchi na hatimaye TANROADS ikaingiza barabara hiyo katika vipaumbele
vyake na kutenga fedha za ujenzi wa kiwango cha lami kiasi cha shilingi
bilioni 1.2.
Aidha, pamoja na kiwango hicho cha
fedha kilichotengwa na TANROADS, tarehe 5 Machi 2012 Mkuu wa Mkoa wa Dar
es salaam alieleza kuwa amewasilisha maombi mengine kupitia Mfuko wa
Barabara (Road Fund) kwa ajili ya ujenzi wa daraja kubwa zaidi katika
barabara hiyo kwenye eneo la Ubungo Kisiwani/External suala ambalo pia
kwa nyakati mbalimbali nilihoji utekelezaji wake.
Izingatiwe
kwamba tarehe 21 Machi 2012 niliunganisha wananchi kuchangia hatua za
dharura za kufanya matengenezo ili kupunguza kero lakini nikasisitza
kuwa suluhisho muhimu zaidi ni kupanua daraja la External katika Eneo la
Ubungo Kisiwani ili kupunguza msongamano wa magari na kujenga barabara
husika kwa kiwango cha lami hatua ambayo sasa inaelekea kuchukuliwa kwa
haraka.
John Mnyika (Mb)
18 Septemba, 2012




