Taarifa Muhimu kwa Umma Kutoka Wizara ya maliasili na utalii

Na: Tulizo Kilaga
Wizara
ya Maliasili na Utalii itawachukulia hatua wale wote watakaokiuka
sheria, kanuni na taratibu zinazotawala utekelezaji wa mchakato wa
kuwapata wawekezaji kwenye vitalu vilivyopo kwenye Maeneo ya Jumuiya ya
Hifadhi za Wanyamapori (WMAs).
Akifungua
warsha ya mafunzo kuhusu mchakato wa kufungua maombi ya uwekezaji
kwenye vitalu vya WMAs iliyofanyika katika Ukumbi wa Blue Peel jijini
Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Paul
Sarakikya alisema mchakato husika utahusisha watu wenye uwezo wa fedha
hivyo unaweza kusababisha uwepo wa mazingira ya rushwa.
Alisema
mchakato huo ni nyeti na unahitaji uadilifu na umakini mkubwa katika
kuutekeleza. Kushindwa kuzingatia vigezo vitakavyokubalika katika
mchakato huo kutasababisha migogoro isiyo ya lazima hivyo kudhoofisha
maendeleo ya Jumuiya na kukatisha tamaa vijiji vilivyotenga maeneo
kuanzisha WMAs.
“Napenda
kusisitiza kuwa, Kanuni za WMAs zinazitaka Jumuiya kufanya uteuzi wa
wawekezaji kwa kutumia vigezo vilevile vilivyotumiwa na Wizara kuwapata
wawekezaji kwa kutumia vigezo vilivile vilivyotumiwa na Wizara kuwapata
wawekezaji kwenye vitalu vyake.
Vigezo
hivyo viko kwenye Kanuni za Uwindaji wa Kitalii (2010) kifungu cha
10(2).
Hivyo washiriki watapata fursa ya kuvipitia na kuviwekea alama kwa
kuzingatia mahitaji na hali halisi ya WMAs, alisema Bw.
Sarakikya.Aliongeza kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii itashirikiana na
vyombo vya dola kufuatilia utekelezaji wa mchakato huu na haitasita
kuwachukulia hatua wale wote walioshindwa kuweka mbele maslahi ya
Jumuiya zao na ya Taifa kwa Ujumla,” alisema Bw. Sarakikya.
Bw. Sarakikya alisema kwa kutambua umuhimu wa mchakato wa ugawaji vitalu
hivyo Wizara ya Maliasli na Utalii imetoa Afisa kutoka Kitengo cha
Matumizi Endelevu ya Wanyamapori ili kutoa mafunzo. Hivyo Wizara
inatarajia wajumbe wote watakubalina na kuhitimisha hatua za kimchakato
zitakazotumika, na hatimaye kuwa na mwongozo utakaotumika na Kamati
zitakazo fungua maombi hayo.
Warsha
ya Mafunzo kuhusu Mchakato wa Kufungua maombi ya uwekezaji kwenye
vitalu kwenye maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori imelenga
kuwawezesha wajumbe kupata uelewa wa pamoja wa nini cha kufanya baada ya
Jumuiya zilizo nyingi kuwa zimepokea maombi ya uwekezaji kwanye vitalu
vya WMAs kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na
Kanuni za WMAs 2012.




