Share this Post

dailyvideo

MAAUMUZI YA MUSEVENI,KAGAME NA UHURU.

Kutoka kushoto ni Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Picha ya Maktaba.

Wiki iliyopita Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Rais wa Rwanda, Paul Kagame walikutana Mombasa nchini Kenya na kuzindua mradi mkubwa wa ujenzi wa reli.
Katika uzinduzi huo marais hao wameweka muda wa kuanza kwa miradi mitatu mikubwa. Mosi kuanza kwa mradi wa ujenzi wa reli kutoka Mombasa-Kampala mpaka Kigali, ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Eldoret-Kampala mpaka Kigali na kujenga miundombinu ya umeme wa uhakika.
Pia wamewaagiza mawaziri wa fedha wa nchi hizo kuandaa mapendekezo ya utekelezaji wa miradi hiyo mitatu na taarifa ya mapendekezo hayo wanatakiwa kuitoa kwa marais hao katika mkutano ujao.
Wanazungumza lugha moja
Kwa mujibu wa mratibu wa miradi hiyo, Monique Mukaruliza, ujenzi wa bomba la kusafisha mafuta kutoka Eldoret-Kampala mpaka Kigali, unatarajiwa kukamilika 2017 huku  kabla ya mwisho mwa mwaka huu, viongozi wa  nchi hizo wamekubaliana kuzindua ushuru wa pamoja wa forodha kwa ajili ya kusafirisha bidhaa kwa masharti nafuu kutoka nchi moja hadi nyingine.
Wakati hayo yakiendelea, taarifa zinaeleza kwamba ujenzi wa reli hiyo utagharimu Dola 3.5 bilioni, lakini taarifa nyingine zinasema kwamba mradi huo una thamani ya Dola 13 bilioni na mradi huo utakamilika mwaka 2018 huku ujenzi wa awali wa mradi wa reli kutoka Mombasa mpaka jijini Nairobi unatarajiwa kuanza Novemba, mwaka huu.
Vilevile kuanzia Januari mwakani,  Rais wa Kenya, Kenyatta na Kagame wamekubaliana kwamba wananchi wao waanze kutumia vitambulisho vya uraia kusafiria katika nchi hizo wakati Uganda itatumia kadi ya kupiga kura kusafiri Kenya na Rwanda.
Mbali na hayo taarifa iliyotolewa hivi karibuni imebainisha kwamba katika mkutano wa pili uliofanyika Mombasa wiki iliyopita, marais hao waliwaagiza mawaziri wa fedha wa nchi hizo kuandaa mapandekezo ya utekelezaji wa miradi hiyo ndani ya mwezi mmoja na nusu ujao.
Wataalamu wa masuala ya uchumi, wanabainisha kwamba reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo na kwenda kilometa 80 kwa saa wakati itakapoanza kusafirisha mizigo katika ukanda huo.
Bandari ya Mombasa, inategemewa kwa zaidi ya asilimia 50 na Rwanda katika kuagiza mizigo huku ikitegemewa na Uganda, Mashariki mwa Demokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Kaskazini mwa mikoa ya Tanzania na Sudani Kusini.
Burundi na Sudani Kusini
Katika mkutano huo marasi wa nchi hizo tatu walikubali kuijumuisha Burundi na Sudani Kusini katika miradi hiyo baada ya kuhudhuria mkutano huo kama wageni waalikwa.
Kutokana na makubaliano hayo ni dhahiri kwamba nchi hizo tano zimekubaliana kufanya kazi pamoja katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wa nchi hizo kiuchumi.
“Wawakilishi wa Burundi na Sudani Kusini wanapaswa kuwa sehemu ya miradi hiyo na hasa katika kamati za ufundi,” inaeleza sehemu taarifa ya mkutano huo.
Mukaruliza anabainisha kwamba Burundi na Sudani Kusini walialikwa kwenye mkutano huo kama watamazaji na baadaye waliomba kuwa sehemu ya kuanzisha miradi hiyo.
Katika mkutano huo Rais Kenyatta alitoa taarifa ya maendeleo ya miradi hiyo baada ya mkutano uliofanyika  Entebbe, Juni mwaka huu.
 “Ninayo furaha kutoa taarifa ya mradi wa bomba la mafuta na katika hatua ya kwanza ya maendeleo ya mradi wa bomba la mafuta, unaendelea vizuri na hatua ya awali tayari imeanza na upembuzi yakinifu umekamilika,” anasema Rais Kenyatta.
Pia Kenyatta anasema kuna changamoto zinazokabili nchi hizo na kwamba wanapaswa kuungana pamoja kwa ajili ya kuzitatua na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kuhusu hati za kuruhusu watu wa Jumuia ya Afrika Mashariki kuingia katika nchi moja hadi nyingine, katika mkutano huo suala hilo lilijadiliwa na mawaziri husika waliagizwa kutoa taarifa kwa nchi ya Kenya, Rwanda na Uganda katika mkutano wa tatu utakaofanyika Oktoba mwaka huu ili mpango huo uanze Januari mosi, mwakani.
Vilevile mawaziri husika wameagizwa kukamilisha mchakato wa kutumia vitambulisho vya uraia kabla ya Oktoba, mwaka huu ili vitumike kama hati rasmi kusafiria katika nchi hizo Januari mosi, mwaka huu.
Katika mkutano huo, Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir Mayardit aliwakilishwa na waziri wake wa masuala nje Dk Barnaba Marial Benjamin wakati waziri wa usafirishaji wa Burundi, Deogratias Rurimunzu alimwakilisha  Rais Pierre Nkurunziza.
Mkutano mwingine utafanyika Oktoba mwaka huu jijini Kigali.
Tanzania
Mwishoni mwa Mei, Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara  nchini Japan aliiomba nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kugharimia ujenzi wa reli mpya kutoka Tanzania kwenda nchi za Rwanda, Burundi  mpaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ombi ambalo Serikali ya nchi hiyo ilikubali.
Rais Kikwete anasema ujenzi wa reli hiyo utarahisisha usafirishaji wa mizigo wa nchi hizo ambazo zinaitegemea bandari ya Dar es Salaam kusafirishia bidhaa zake.
Taarifa zinasema Kampuni ya Burlington Northern Santa Fe Railway ya Marekani ndiyo itakayofanya ukarabati huo ambao utahusisha ujenzi wa reli mpya kutoka Isaka hadi Kigali ambayo pia itaunganisha Jiji la Bujumbura, Burundi. 
Hata hivyo uzinduzi wa mradi wa reli ya Mombasa-Kigali, huku Rwanda na Uganda zikitishia kujitoa kutumia bandari ya Dar es Salaam unaacha maswali mengi.
Mwananchi

Posted by Editor on 20:12. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for MAAUMUZI YA MUSEVENI,KAGAME NA UHURU.

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery