TAARIFA: MAADHIMISHO YA SIKU YA NDEGE WAHAMAO DUNIANI TAREHE 10 – 11 MEI 2014
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
MAADHIMISHO YA SIKU YA NDEGE WAHAMAO DUNIANI
TAREHE 10 – 11 MEI 2014
Maadhimisho ya Siku ya Ndege Wahamao Duniani ni siku ambayo huadhimishwa kimataifa kila mwaka tarehe 10 na 11 Mei.
Wizara
ya Maliasili na Utalii inawashauri wananchi wanaoishi karibu na maeneo
ya Ardhi oevu ambayo ni makazi na mapito ya ndege wahamao kushirikiana
na Serikali katika kuwalinda ndege hao na kuhifadhi mapito na makazi
yao.Wananchi
pia wanakumbushwa kuwa maeneo ya ardhioevu ndio vyanzo vya maji ambayo
yanafaa kwa matumizi ya kila siku ya binadamu, wanyama na ndege, hivyo
maeneo hayo ni vyema yalindwe kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Kuna
aina nyingi za ndege maji na wahamao. Aina za ndege hao ni kama vile
Heroe mkubwa na mdogo (flamingos) ambao wanahama kila mwaka kutoka
sehemu moja ya dunia kwenda nyingine kutafuta malisho, maji, kukwepa
hali mbaya ya hewa na kupata sehemu salama ya kuzaliana.
Tanzania
ni nchi mojawapo yenye sehemu nyingi ambazo ni salama kwa mazalia ya
ndege. Kwa mfano, Ziwa Natron ni maarufu kwa mazalia ya ndege aitwaye
Heroe mdogo. Inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya Heroe mdogo kote duniani
huzalia katika Ziwa Natron liliko Kaskazini mwa Tanzania. Ziwa hilo ni
kivutio cha utalii kutokana na ndege, wanyamapori na mandhari ya Ziwa.
Maadhimisho
ya Siku ya Ndege Wahamao Duniani yalianza mwaka 2006 na kuendelea
kusherehekewa kila mwaka mwishoni mwa wiki ya pili ya kila mwezi Mei.
Watu duniani kote huitumia fursa hii kutoa elimu na kufanya matembezi
katika sehemu zenye Ndege hawa kwa ajili ya kusherehekea siku hii. Kwa
mwaka huu Wizara ya Maliasili itafanya maadhimisho hayo Katika Eneo la
Ramsar la Ziwa Natron lililopo Mkoani Arusha. Eneo hili lina umuhimu wa
ndege wahamao aina ya Heroe mdogo.
Ujumbe wa mwaka huu wa Siku ya Ndege Wahamao ni: “Mahali Wanapofikia Ndege Wahamao na Utalii (Destination Flyways; Migratory Birds and Tourism), “. Tafsiri
ya ujumbe huu ni kuwa nchi, mashirika na watu binafsi wanatakiwa
kutunza maeneo wanapolazimika kufikia ndege wahamao kwa kila mwaka kwa
ajili ya uhifadhi endelevu wa ndege hao pamoja na kusaidia jamii
kutambua umuhimu wa ndege hao katika kuvutia utalii.
Utunzaji
wa ndege wahamao ni sababu mojawapo iliyofanya Tanzania kusaini Mkataba
wa Uhifadhi wa Ardhioevu (Ramsar) mwaka 2000. Ardhioevu, pamoja na
maufaa mengine ikiwepo maji, chakula, kurekebisha hali ya hewa,
kusafisha maji machafu na kuzuia mafuriko pia ni makazi ya wanyamapori
wakiwemo ndege wahamao.
Kutokana
na Mkataba huo Tanzania imetenga maeneo ya Ramsar ambayo ni muhimu
katika kuhifadhi bioanuwai. Maeneo ya ardhioevu yaliyotengwa hususani
kwa uhifadhi wa ndege ni pamoja na Ardhioevu zenye umuhimu wa kimataifa
kama vile:- Malagarasi-Muyovozi ambayo ni muhimu kwa uhifadhi wa ndege
aina ya Korongo domokiatu (Shoebill stork), na eneo la Ramsar la Ziwa
Natron ambalo ni muhimu katika kuhifadhi ndege aina ya Heroe mdogo
(lesser flamingo).
Serikali
imekuwa ikiwajengea wananchi uwezo wa kuhifadhi na kutumia rasilimali
za ardhioevu nchini kwa kutoa elimu ya uhifadhi katika maeneo
yanayozunguka maeneo ya Ramsa. Maeneo hayo ambayo ni makazi muhimu ya
ndege wahamao yanasimamiwa na Sheria ya Kuhifadhi Mazingira ya mwaka
2004 na ya Kuhifadhi Wanyamapori ya Mwaka 2009.
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
9 Mei 2014

