Viongozi wa Umoja wa ulaya wakutana kwa dharura Brussels
Waziri mkuu wa Italia atahitaji lakini uungaji mkono wa viongozi wenzake pamoja pia na ule wa kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambao bado si dhahir.
"Kupata nguvu makundi yanayoupinga umoja wa ulaya ni jambo la kusikitisha-kilichobakia ni kuwazinduwa wapiga kura kupitia sera zitakazopalilia mashindano ya kiuchumi,zitakazochochea ukuaji wa kiuchumi na kubuni nafasi zaidi za kazi-hilo likiwa jibu bora zaidi kwa hasira za wapigakura." Amesema kansela Angela Merkel.
La muhimu anahisi waziri mkuu wa Italia ni kuwachagua viongozi wepya wa Umoja wa Ulaya ili kuweza kupanga ratiba ya mikakati itakayosaidia kubuni nafasi zaidi za kazi na kushughulikia wimbi la wakimbizi.
Malengo yanatofautiana na kiongozi huyo kijana wa Italia atajaribu kutafuta uungaji mkono wa rais Francois Hollande wa Ufarasa.Lakini kiongozi huyo wa kasri la Elysee anafika Brussels akiwa katika hali ya unyonge,akidhoofishwa kwa ushindi mkubwa wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Front National FN.Chama hicho kinachoongozwa na wakili Marine Le Pen kinataka kulazimisha sera zake zifuatwe na hasa kuhusu suala la uhamiaji.
Mageuzi ya sera za umoja wa ulaya hayawezekani kabla ya kwanza kuteuliwa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya umoja wa Ulaya.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya watalizungumzia suala la nani ateuliwe kumrithi Barroso katika kikao chao leo usiku mjini Brussels.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Josephat Charo
DW SWAHILI
