Mkutano dhidi ya mabomu ya ardhini waendelea Msumbiji
Ikiwa unatukio Lolote au Habari yoyote usisite kututumia kupitia Barua Pepe blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba yetu +255765056399
Msumbiji ilikuwa nchi ya tano duniani ambayo ina mabomu mengi zaidi yaliyotegwa ardhini , ambayo hivi sasa inakaribia kuwa haina tena mabomu hayo.Hadi mwishoni mwa mwaka huu serikali ya Msumbiji inataka kuyaondoa mabomu mengine 303 yaliyobaki katika maeneo ya nchi hiyo. Eneo ambalo ni kubwa kama mji mkuu Maputo bado kazi ya kuyaondoa mabomu hayo inaendelea.
Mabomu yatakuwa yameondolewa hadi mwishoni mwa mwaka huu
Kuanzia mwaka 2007 kiasi ya mabomu 100,000 yameondolewa katika majimbo kadha ya nchi hiyo. Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Msumbiji Henrique Banze anaamini kuwa kazi ya kuyaondoa mabomu hayo inawezekana kumalizika hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Hakuna mtu aliyefikiria kuwa inawezekana kuyaondoa mabomu yote yaliyozikwa ardhini ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014.Lakini kutokana na ushirikiano wa mashirika yasiyo ya kiserikali , wafadhili wa kimataifa na serikali ya Msumbiji suala hilo lilifanikishwa na hivi sasa kila mtu anaweza kutembea bila ya kuwa na wasi wasi wa kuripuka bomu la kutegwa ardhini nchini humo.
Rais wa Msumbiji Armando Guebuza ametoa shukurani kwa wafadhili wa kimataifa katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo mjini Maputo jana.
"Tunataka kutumia fursa hii, kuiomba jumuiya ya kumataifa kuchukua hatua madhubuti , ili kuiondolea Msumbiji mabomu yote ya kutegwa ardhini.Utekelezaji wa mkataba wa Ottawa umeleta matokeo mazuri. Sasa tunataka kuelekea katika njia ambayo dunia nzima ifaidike na matokeo haya ili kutokomeza kabisa biashara ya mabomu ya kutegwa ardhini na kuyaondoa mabomu yote yaliyotegwa ardhini."
Marekani haijasaini
Hata hivyo Marekani bado haijatia saini mkataba wa kimataifa wa kupiga marufuku mabomu ya kutegwa ardhini ambao umetiwa saini na mataifa 160. Nchi zilizotia saini mkataba huo wa kupiga marufuku mabomu ya kutegwa ardhini zinatakiwa kuweka nia ya kuhakikisha majeshi yote duniani hayatumii tena mabomu ya kutegwa ardhini ifikapo mwaka 2025.
Lakini Marekani, Urusi na China , pamoja na mataifa yenye silaha za kinyuklia kama India na Pakistan, hayajatia saini mkataba unaopiga marufuku matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini, mabomu ambayo yanasababisha maafa makubwa kwa raia hata baada ya miaka kadha kumalizika vita.
Katika mwaka 2009 , Marekani imesema inaangalia upya msimamo wake kuhusu mabomu hayo lakini imeshindwa kutia saini mkataba huo licha ya mbinyo mkali kutoka kwa makundi yanayofanya kampeni ya kusitishwa kwa matumizi ya mabomu hayo.
Kundi linalofanya kampeni ya kupigwa marufuku kwa mabomu hayo limesema kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanywa hadi dunia iondokane kabisa na mabomu hayo.
"Muda sasa umefika wa kukamilisha kazi hii na tuifanye katika muda wa miaka 10," kundi linalofanya kampeni ya kimataifa ya kupiga marufuku mabomu ya kutegwa ardhini (ICBL) limesema katika taarifa yake.
Mwandishi: Romeu da Silva / ZR / afpe / Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman
