Share this Post

dailyvideo

Chadema kutoshiriki uchaguzi Bububu






Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakiwa wamesusia uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu, vyama nane vimejitokeza kugombea nafasi hiyo.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha mwakilishi wa zamani Salum Amour Mtondoo, kilichotokea Februari 14, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, vyama vilivyojitokeza kusimamisha wagombea ni CCM, CUF, Tadea, Sau, NCCR-Mageuzi, Jahazi asilia, AFP, na NRA.

Naibu katibu Mkuu wa Chadema, Hamad Mussa Yussuf, akitoa tamko la chama chake kususia uchaguzi huo, alisema umepangwa kufanyika bila kuandikishwa wapiga kura wapya.



Hamad alisema kuna vijana wengi katika jimbo la Bububu wamefikisha umri wa kupiga kura lakini wamenyimwa fursa hiyo kwa kutoandikishwa.

Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Sululu Rashid Ali, alisema uchaguzi huo utafanyika bila ya kuandikisha wapiga kura wapya kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

“Uchaguzi utafanyika kwa kuwashirikisha wapiga kura waliomo katika daftari la kudumu la mwaka 2010,” alisema Sululu.

Hamad akifafanua uamuzi wa chama chake kususia uchaguzi huo, alisema kwa mujibu wa Ibara ya 21 (2) ya Katiba ya Zanzibar,  kila Mzanzibari anayo haki na uhuru kushiriki katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayohusu yeye maisha yake au yanalolihusu Taifa.

Alisema kwa kuzingatia msingi wa haki hiyo, ZEC ilipaswa kuandikisha watu waliofikia miaka 18 ambao kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010 hawakuwa na umri huo.

Hamad alisema chama hicho kinaona hatua ya ZEC kutoandikisha wapiga kura wapya ni mazoea kwa sababu hata uchaguzi mdogo wa jimbo la Uzini, ulifanyika bila ya kuandikisha wapigakura wapya ingawa chama chake kilishiriki na kushika nafasi ya pili katika uchaguzi huo.

Wagombea wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo na vyama vyao kwenye mabano ni Issa Khamis Issa (CUF), Hussen Ibrahim Makungu (CCM), Seif Salim Seif (Tadea), Juma Metu Domo (SAU), Haroun  Abdalla Said (NCCR-Mageuzi), Mtumweni Jabir Seif (Jahazi Asilia), Abubakar Hamad Said (AFP) na Suleiman M Abdalla (NRA).

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Septemba 16, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

Posted by Editor on 12:09. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for Chadema kutoshiriki uchaguzi Bububu

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery