Share this Post

dailyvideo

Mauaji tena

  Polisi watumia nguvu kuvunja maandamano   Wengine wajeruhiwa, risasi, mabomu vyarindima

Mji wa Morogoro na viunga vyake jana uligeuka kuwa uwanja wa mapambano hali iliyolazimisha shughuli mbalimbali kusimama kwa saa kadhaa, zikiwemo ofisi na maduka kufungwa kwa muda baada ya Jeshi la Polisi kurusha mabomu ya machozi na risasi za moto ili kudhibiti maandamano ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Mapambano hayo yalisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine wawili kujeruhiwa sehemu mbali mbali za miili yao baada ya kupigwa risasi na askari wa Jeshi hilo wakati wa kudhibiti maandamano hayo yaliyokuwa yakipita katika mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro kabla ya kuelekea katika uwanja wa mkutano wa Operesheni Sangara uliokuwa ukifanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Kiwanja cha Ndege. Jeshi la Polisi lilitumia nguvu kubwa kuzuia maandamano ya Chadema yaliyoanzia katika eneo la Lupira jirani na kituo kikuu cha stendi ya mabasi Msamvu kuelekea katika eneo la mkutano. Aliyeuawa hakuwa mwandamanaji na alitambuliwa kwa jina la Ally Nzona muuza magazeti wa mjini hapa. Marehemu anadaiwa kupigwa risasi na polisi katika eneo la nyuma ya kichwa akiwa anasoma gazeti katika meza aliyokuwa akitumia kuuzia magazeti. Waliojeruhiwa katika vurugu hizo walitambuliwa kwa majina ya Frank Mbalimba, mkazi wa Msamvu na Hashim Seif. Ndugu wa marehemu aliyejitambulisha kwa waandishi wa habari  kwa jina la Ally Athumani, alisema wakati akiwa amekaa na ndugu yake katika eneo la  kwa Bene, waliona gari la polisi aina ya Land Rover Defender lenye rangi nyeupe likiwasogelea na ghafla askari mmoja alivyatua risasi iliyompata mwenzake katika eneo la nyuma ya kichwa (kichogo). “Sisi hatukushiriki katika maandamano, tulikuwa tunajitafutia riziki yetu kwa kuuza magazeti ndiyo maana hata walipotusogelea hatukuona sababu ya kuwakimbia, ghafla askari alitupa risasi ikampata ndugu yangu, masikini wamemuuwa ndugu yangu,” alisimulia Athumani huku akilia. Kabla ya Jeshi la Polisi kuanza kufyatua risasi majira ya saa tano asubuhi, walimzuia kwa muda mkuu wa Operesheni Sangara wa Chadema, Benson Kigaila, pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Zanzibar, Hamad Yusuph, hali iliyoamsha ari ya vijana kutoka maeneo mbali mbali kuingia barabarani wakiwa na mabango ya kulaani hatua hiyo. Miongoni mwa waliokamatwa ni mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Abdallah Khamis, ambaye alikuwa akipiga picha za matukio hayo, ingawa baadaye aliachiwa. Hata hivyo, baadaye kiongozi wa Polisi aliyekuwa katika eneo hilo alitangaza hali ya hatari na kuwataka wananchi watawanyike, amri ambayo haikutekelezwa na wananchi walioamua kuingia barabarani wakiwa na magari, pikipiki na baiskeli huku wengine wakitembea kwa miguu kuelekea katika eneo la mkutano. Kutokana na hatua hiyo, askari waliokuwa katika magari zaidi ya 10, walianza kurusha risasi na mabaomu ya machozi hali iliyowafanya wananchi wakimbie kwa muda na kisha kurudi tena barabarani. Hali hiyo iliwafanya askari waliokuwapo kuanza kuyasindikiza maandamano hayo kwa utaratibu hadi walipofika eneo alilokuwepo mkuu wao aliyetambuliwa kwa jina la Z. M Mukiko, ambaye aliwaamuru askari hao kuendelea na kamatamakata pamoja na kurusha risasi na mabomu. Matukio ya kukamata kamata yaliendelea hadi kuwakumba wafanyabiashara waliokuwa pembezoni mwa barabara ya Kisunyale, wengi wao wakiwa ni wauza vyakula (baba lishe). Jitihada za Jeshi la Polisi kuzuia maandamano hayo ilianza kufifia baada ya askari waliokuwa katika kazi hiyo kuishiwa mabomu ya machozi na kulazimika kutumia baruti pekee, hali iliyowafanya wananchi wazomee kwa kuimba “People’s Power”, risasi haziwezi kuzuia nguvu ya umma.” Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Godfrey Mtei, alipopigiwa simu kwa ajili ya kueleza idadi ya watu waliojeruhiwa na waliofariki, alisema kuwa alikuwa kwenye msiba hivyo hakuwa na taarifa rasmi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na wengine kujeruhiwa. Kamanda Shilogile alisema kuwa Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi ili kujua kama risasi zilizotumika kuua zilifyatuliwa na askari wake. SLAA: POLISI WAMEUA DEMOKRASIA Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, alisema Polisi mkoani Morogoro limeitangazia dunia kuwa Tanzania hakuna demokrasia na kwamba sasa kuna jukumu la kupigania uwepo wa demokrasia nchini Alisema hujuma za Polisi kwa Chadema zilianza siku nyingi na jana wamedhihirisha hujuma yao kwa kuamua kurusha risasi na kumuua Kijana Ally Nzona. Akizungumza na umati wa wananchi katika uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Dk Slaa alisema baada ya amri ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, Faustine Shilogile,  askari walio chini yake wanasita kuchukua dhambi ya kufyatua risasi na mabomu kwa wananchi. Alisema hata barua zinazoandikwa na polisi zinaonyesha kuwa ni watu wasiojua majukumu yao. Alisema barua waliyoandika inaonyesha kama wametoa kibali cha maandamano wakati jukumu lao linatakiwa libakie kuwa ni la kulinda na siyo kuruhusu mikutano ya vyama vya siasa. Alisema Kamanda wa Polisi mkoani humo hajui hata madhumuni ya mandamano kuwa ni kuungwa mkono na watu, hivyo wanaposema watu wataacha kazi haileti mantiki katika akili ya kawaida. “Hivi maandamano yanafanyiwa porini, hii ndilo tatizo la kuwa na viongozi wa kupachikwa pachikwa nami nina shaka nao kama akili zao zinafanya kazi sawa sawa kwa kuwa pasipokuwa na watu hakuna maandamano,” alisema Dk Slaa. Alisema sheria ya kukataa maandanmano inaainisha sababu ambazo zinaweza kutatulika na kwamba kuwaambia barabara hazitoshi ni kuamua kufinya demokrasia. ISSA: TUPIGE TAKBIR Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, akihutubia umati wa wananchi alisema asubuhi ya jana akiwa anazungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ilifikia wakati wakashikana mashati kwa sababu ya kutetea maslahi ya aliyowaita vibaraka wa CCM. Akizungumza huku akitumia aya mbali mbali za Koran, Issa Mohamed alisema kama Jeshi la Polisi linatumia posho wanazopewa na watu wanaotaka kulinda nafasi zao za ubunge kwa nguvu ya risasi, basi yeye yupo tayari kumwaga damu kwa ajili ya Watanzania. “Tunajua huyu kamanda anatumika nami ninawaambieni mwanafalsafa mmoja wa Kiarabu alisema kama ukiona mtu anafikishiwa elimu na hanufaiki na elimu hiyo basi mtu huyo apigiwe takbir nne kwa kuwa atakuwa hana tofauti na maiti, nami nawaambieni Morogoro msiwe hivyo,” alisema Mohamed Issa. MNYIKA: POLISI, CCM WASHIRIKA Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema CCM baada ya kuona mbinu yao ya kuandaa kufanya fujo katika mikutano ya Chadema imejulikana, wameamua kushirikiana na Jeshi la Polisi kutekeleza mkakati wao wa mauaji. Alisema mipango mingi iliyokuwa ikifanywa na CCM dhidi ya Chadema imekuwa ikijulikana na sasa wanaona njia sahihi ni kuwatumia makamanda wa Polisi wanaonunulika. LISSU AAHIDI KUMFUATA SHILOGILE  Tundu Lissu, Mkurugenzi wa Haki na Sheria Chadema, alisema suala la kuandamana halijawahi kuwa kosa la jinai ambalo adhabu yake ni kifo, kama ilivyotokea kwa kijana aliyeuawa na polisi. Alisema hakuna damu ya Mtanzania aliyeuliwa bure kuwa itasahaulika, hata kama hao wanaowaamuru polisi kwa kudhani wataishi milele. Alieleza kuwa wanasheria watamfuata Kamanda Shilogile popote alipo iwe amevaa sare au amevua kwa ajili ya kuulezea umma wa Watanzania kwa nini alimuuwa Ally Nzona. “Tunawaambia tutawafuata popote walipo watuambie kwa nini wameamua kumwaga damu ya Watanzania, vilio vyetu havitapita hivi hivi leo na hata kesho,” alisema Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema). CHADEMA KUBEBA MSIBA   Wakati huo huo, Kamanda wa Operesheni kwenye vuguvugu la mabadiliko (M4C) itakayoifikisha chama hicho katika mikoa mitano, Benson Kigaila, alisema Chadema itachukua majukumu ya msiba wa Ally Nzona pamoja na kushughulikia matibabu ya waliojeruhiwa.
CHANZO: NIPASHE

Posted by Editor on 12:18. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for Mauaji tena

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery