Neno La Mjengwa: CCM Na Sifa Ya Mchawi!
Ndugu zangu,
Usiku wa saa sita umeingia tena hapa Iringa. Kabla sijaondoka kwenye meza ya kibarua changu nina neno fupi la usiku.
Naam, inasemwa, kuwa mchawi mchukie, lakini, sifa yake mpe, anajua kuroga!
Majuzi
hapa nilipokuwa kwenye shughuli za kijamii kijijini Mahango, Madibira,
kuna kitu kilichonifanya nishangae, lakini, baada ya tafakuri nikauona
ubunifu kwa aliyekitenda.
Nikiri,
kuwa huko nyuma nimefanya vikao kadhaa na Kamati ya Shule ya Mahango
chini ya Uenyekiti wa Bw. Victor Kadama ( Pichani). Sikupata kujua kuwa
Victor Kadama, mbali ya kuwa Mwenyekiti wa kamati ya Shule, pia ni
Katibu Mwenezi wa CCM, Kata ya Madibira. Ndio, Victor Kadama ndiye Nape
Nnauye wa Madibira.
Maana,
kwenye vikao vyetu hakuwahi hata siku moja kuvaa nguo za rangi ya chama
chake wala kofia. Lakini, majuzi hapa tulipokuwa na mkusanyiko mkubwa
wa wanakijiji kuwapokea wageni kutoka Norwich, Uingereza waliokuja
kuzindua mradi wa ujenzi wa Maktaba ya Kijamii kijijini hapo, basi, kwa
siku mbili mfululizo, nilimwona Bw. Victor Kadama akiwa ametinga kofia
ya chama chake, CCM.
Bw.
Kadama kwa siku zote mbili hakuongea hata neno moja kuhusu chama
chake, lakini, kofia yake ilikuwa inaongea. Kulikuwa na uwepo wa CCM
kupitia kwa kofia ya Kadama. Na hata wageni waipopangiwa ziara ya miguu
kuona mazingira ya kijiji, Victor Kadama na kofia yake haraka alichukua
jukumu la kuongoza msafara. Aliendelea kufanya ' kazi ya uenezi' wa
Chama chake.
Kwa
vyama vingine vya siasa kuna ya kujifunza kutoka kwa CCM. Pamoja na
dhambi zao zote, CCM bado wana oganaizesheni inayoeleweka na yenye
kufikia hadi ngazi za vitongoji. Ni mtaji wao mkubwa kisiasa. Tofauti na
vyama vingine, makada wa CCM wanajipenyeza kila mahali, iwe kwenye
kamati za shule au za kuchimba visima. Ndio, hata, uwe na harusi ya
mwanao, bado kuna makada wa CCM watakaojipenyeza kwenye Kamati za
harusi.
Naam, mchawi mchukie, lakini sifa yake mpe, anajua kuroga, hakyamungu!
Maggid,
Iringa.
0788 111 765
Posted by Editor
on 12:00.
Filed under
eastafricannews
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0