SITA AITAKA CCM IJIPANGE IGUNGA NA KUHESHIMU MAAMUZI YA MAHAKAMA
SIKU moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, kutengua matokeo ya uchaguzi ya Jimbo la Igunga, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mbunge wa Jimbo la Urambo mkoani Tabora kwa tiketi ya CCM, Bw.Samuel Sitta, amewataka wana-CCM kuheshimu uamuzi huo na kuendelea kujipanga.
Bw.Sitta aliyasema hayo jana mjini Tabora, wakati akikabidhi kompyuta na mashine ya kutolea nakala (printer) kwa Umoja wa Vijana wa Kanisa Katoliki (VIWAWA) zenye thamani ya sh.milioni 2.5.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Bw.Sitta alisema Mahakama ina mamlaka yake kisheria wana-CCM hawana budi kuyaheshimu maamuzi hayo.
"Kama kuna mtu anaona hukumu hiyo haikutenda haki, anaweza kwenda mahakamani kukata rufaa, lakini mimi nashauri ni vyema tujipange upya tuingie ulingoni," alisema, Bw.Sitta na kuongeza;
"Ni vyema tukakaa na kutafakari yaliyotokea huko Igunga, ili basi
tukiona inafaa kukata rufaa sawa, au kama tunaingia ulingoni yote ni sawa."
Kwa upande wa Ofisi ya Bunge imesikitishwa na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Igunga, Dkt.Peter Kafumu, kuvuliwa wadhifa huo, hasa kwa kuzingatia alikuwa mtu mtaratibu na mpole sana.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Spika wa Bunge, Bw.Job Ndugai, alipoulizwa na gazeti hili jana jisi ofisi yake ilivyopokea uamuzi huo wa mahakama.
Bw.Ndugai alisema; "Tunaheshimu maamuzi ya mahakakama, lakini kitendo cha kuvuliwa ubunge Dkt.Kafumu kimenisikitisha kwani kwa jinsi ninavyomjua hana maneno na mtu."
Alisema kutokana na hukumu hiyo ni wakati mzuri wa watu wengine kujifunza, wakishindwa waheshimu uamuzi unaotolewa na si kuanza kutoa sababu mbalimbali.
Kwa upande wa wanasiasa waliozungumzia hukumu hiyo, walisifu uamuzi huo, wakisema umelenga kupanua wigo wa demokrasia nchini.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Bw.Augustino Mrema alisema, hukumu hiyo itatoa fundisho kwa wanasiasa wenye tabia ya kukiuka sheria za uchaguzi na kuwa waadilifu.
"Nimesifu sana uamuzi wa Jaji Shangali (Mary Shangali) hukumu hii itaondoa vitendo vya wanasiasa kutoa rushwa kwa wapiga kura wakati wa uchaguzi na jambo hili linatokana na viongozi wetu kutokuwa na maadili," alisema.
Alisema CCM inapaswa kukubali kujifunza kuwa waadilifu, wacha Mungu na kuachana na sera za kusema ovyo pindi wanapokuwa majukwaani, ili kuepusha gharama zisizo za lazima pindi matokeo yanapotenguliwa.
"Tatizo CCM hawako tayari kukubali mabadiliko na wanatupeleka katika hali ngumu ya maisha kutokana na kuiingiza nchi katika gharama, wasiwe watu wa kujivunia utajiri wa fedha walizonazo kwa kuwa eti wana Serikali, hii ni hatari kubwa," alisisitiza Bw.Mrema.
Naye Naibu Mkurugenzi Habari na Uenezi wa Chama cha Wananchi(CUF), Bw.Abdul Kambaya, alisema hukumu hiyo ni fundisho kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuanza kusimamia sheria za uchaguzi na kuweka pembeni nyazifa za viongozi walioko serikalini kutoshiriki katika uchaguzi.
"Nilikuwepo wakati wa uchaguzi huo, ni mengi yaliyofanywa na CCM, lakini hata CHADEMA iwapo wangeshinda nao ushindi wao ungepingwa mahakamani kwani pia walihusika katika kampeni chafu," alisema.
"Naishauri Serikali kuchunga rasilimali zake, fedha nyingi zinapotea bure wakati wa uchaguzi huku walimu na madaktari wakigoma kila siku kutokana na masilahi duni ya mishahara na wanafunzi nao wakilalamikia kutopatiwa huduma bora zinazotakiwa kama vile vitabu na walimu wa kutosha," alisema.
Alipoulizwa kama chama chake kitashiriki uchaguzi mdogo iwapo utaitishwa jimboni humo, Bw.Kambaya alisema,vikao vya Chama hicho ndivyo vitakavyoamua.
Ofisa wa Idara ya Elimu na Habari wa NEC, Bi.Luth Mashamu,ilipoulizwa kuhusu hukumu hiyo alisema hawajapata taarifa rasmi, licha ya kuzipata kupitia vyombo vya habari nchini.
"Hatuwezi kulizungumzia suala hilo kwani hatujapata rasmi nakala ya hukumu hiyo, tunasubiri tuletewe (hukumu) ikiwa ni pamoja na barua ya kuiarifu Tume kutoka kwa Spika wa Bunge juu ya nafasi hiyo kuwa wazi, lakini bado hiki ni kipindi cha kutafakari kwa aliyeenguliwa kwa kuwa naye ana haki yake huenda akakata rufaa," alisema ofisa huyo.
Wakati huo huo CCM imesema inatafakari kama itakata rufaa Mahakama Kuu ili kupinga uamuzi wa kutengua matokeo yaliyompatia ushindi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia chama hicho, Dkt.Kafumu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, alisema kuwa chama hicho kimetafakari na kitatoa uamuzi iwapo kitakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
"Chama kimetafakari hukumu ya kesi ya uchaguzi iliyotolewa Agosti 21, mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, kimejiridhisha kitachukua uamuzi wa kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kesi ya uchaguzi, dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora, Dkt.Kafumu," alisema Bw.Nnauye.
Posted by Editor
on 15:25.
Filed under
eastafricannews
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0