Share this Post

dailyvideo

KITUO CHA AFYA CHAKATIWA UMEME, WAJAWAZITO WAJIFUNGUA NA CHEMLI.


Baadhi ya majengo ya Kituo cha Afya kilichopo Kata ya Songwa, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kama linavyoonekana pichani.
Ofisa Tabibu wa Kituo cha Afya Songwa, Bundala Nandule.
Na Joachim Mushi, Thehabari.com-Kishapu
Kituo cha Afya kilichopo Kata ya Songwa, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kimekatiwa umeme kwa takribani miezi saba sasa kikidaiwa bili ya umeme na TANESCO ya jumla ya sh. 38,000 hali inayowabebesha mzigo wa gharama wananchi wanaofika kupata huduma kituoni hapo.
Wagonjwa wanaotibiwa usiku katika kituo hicho hasa wanawake wajawazito wanalazimika kugharamia mafuta ya taa kwenye chemli za kituo au kuchangia sh. 1200 kabla ya huduma yoyoto ili kupatikana mwanga unaowawezesha wahudumu kufanya kazi zao usiku.
Akizungumza na Thehabari.com kijijini Songwa, Jamila Nyalulu mkazi wa eneo hilo alisema wananchi wasio na uwezo wa kuchangia mafuta ya taa hasa kwa huduma za uzazi wamekuwa wakipata tabu, jambo ambalo limekuwa likihatarisha maisha yao kiafya.
Ofisa Tabibu wa Kituo hicho, Bundala Nandule amekiri hali hiyo inakwamisha ufanisi wa utoaji huduma za afya hasa kwa wagonjwa wa usiku au wanaopumzishwa na kuongeza kuwa tarari wameripoti suala hilo katika uongozi wa Halmashauri ya Kishapu lakini bado linafanyiwa kazi.
“Tatizo la umeme linatusumbua kwa kweli hasa mgonjwa anapokuja kupata huduma usiku. Wagonjwa wa kawaida hulazimika kuja na tochi, lakini kwa wajawazito wanatakiwa kuja na fanta moja (chupa ya soda) ya mafuta ya taa au aje na sh. 1200 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta hayo kabla ya huduma,” alisema Nandule.
Hata hivyo akizungumzia tatizo hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kishapu, Lucas Said alisema wanamshangaa Mkuu wa Kituo hicho cha afya kushindwa kufuatilia malipo ya bili katika ofisi za halmashauri kwani cheki ya malipo ya bili hiyo iliandikwa tangu mwaka jana (2011).
“Kituo hicho kilikuwa kinadaiwa sh. 38,000 na cheki iliandikwa tangu mwaka jana lakini wahusika hawajatokea ili wakabidhiwe cheki hiyo…huu ni uzembe,” alisema kiongozi huyo wa Halmashauri ya Kishapu.
Kituo cha afya cha Songwa kinatoa huduma kwa zaidi ya vijiji vitatu vya Wilaya ya Kishapu, ambavyo ni pamoja na Kijiji cha Songwa, Bushola, Seseko na baadhi ya zahanati zilizopo jirani na kituo hicho.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

Posted by Editor on 12:33. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for KITUO CHA AFYA CHAKATIWA UMEME, WAJAWAZITO WAJIFUNGUA NA CHEMLI.

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery