Share this Post

dailyvideo

NIGERIA: Juhudi za kimataifa zaongezeka kuwaokoa wasichana wa Nigeria


Juhudi za kimataifa za kuwaokoa wasichana zaidi ya mia mbili waliotekwa nyara Nigeria na kundi la waasi la Boko Haram zimeongezeka huku nchi mbali mbali zikijitolea kusadia katika shughuli ya uokozi
Ni wiki ya nne sasa tangu wasichana hao 223 walipotekwa nyara na kundi la Boko Haram katika shule moja ya upili iliyoko katika mji wa Chibok katika jimbo la Borno kaskazini mwa Nigeria na mpaka sasa hawajaweza kuokolewa.
Hata hivyo nchi kadhaa zimeahidi kuisaidia Nigeria kuwatafuta wasichana hao huku Israel ikiwa nchi ya hivi punde kutangaza kuwa itashirikiana na nyingine kuwatafuta.
Israel kuisaidia Nigeria
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan hapo jana alizungumza kwa njia ya simu na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kukubali kupokea msaada wa Israel wa kuimarisha operesheni za kukabaliana na ugaidi katika kuwatafuta wasichana hao.
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan
Uingereza,Marekani na Ufaransa tayari zimeshatuma makundi ya wataalamu na vifaa kulisaidia jeshi la Nigeria katika kuwatafuta wasichana hao katika maeneo ya ndani ndani ya kaskazini mwa Nigeria ambayo yamekumbwa na visa vya uasi kwa miaka mitano sasa.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande ametangaza kuwa nchi yake iko tayari kuandaa mkutano wa kilele mjini Paris Jumamosi hii utakaozileta pamoja nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika kujadili kitisho cha kundi la Boko Haram na jinsi ya kukabiliana nalo iwapo nchi husika zitakubaliana na pendekezo lake.
Duru zinaarifu kuwa viongozi wa nchi za Nigeria, Chad, Cameroon, Niger na Benin huenda wakakubali kuuhudhuria mkutano huo.
Rais Jonathan amesema anaamini kuwa wasichana hao bado wako nchini Nigeria na kwamba watapatikana kufuatia juhudi hizo za kimataifa.Kuna hofu hata hivyo huenda wasichana hao wamevushwa mpaka na kuingizwa katika nchi jirani za Chad na Cameroon.
Watu mashuhuri duniani walaani utekaji nyara
Baadhi ya watu mashuhuri pia wamejitokeza kulaani utekaji nyara huo hasa baada ya kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau kuonekana katika mkanda wa video akisema kuwa atawauza wasichana hao kama watumwa.
Mke wa Rais wa Marekani Michelle Obama Mke wa Rais wa Marekani Michelle Obama
Miongoni mwa watu mashuhuri waliojitokeza kuunga mkono juhudi za kuokolewa kwa wasichana hao ni mke wa rais wa Marekani Michelle Obama ambaye alisema siku ya Jumamosi kuwa Marekani itafanya kila juhudi kuhakikisha wasichana hao wameokolewa na kurejeshwa makwao.
Mjane wa rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela,Bi Graca Machel pia amejitokeza kuwafariji wasiachana hao na familia zao na kuwataka wasife moyo huku wakisubiri usaidizi kuwafikia.
Katika taarifa iliyotolewa na Bi Machel, amesema amekiuka taratibu za kimila za kumtaka kutoonekana au kusikika hadharani ili kuomboleza kifo cha mumewe kujaribu kuwatia moyo wasichana hao kwa kuwapitishia ujumbe kuwa wanapendwa na kwamba ana imani hata marehemu mumewe ataridhishwa na yeye kuvunja mila kuwahimiza wasichana hao.
Kiongozi wa kanisa la kianglikana duniani askofu mkuu wa Canterbury Justin Welby ameonya kuwa wasichana hao wako katika mikono hatari ya kundi ambalo halina huruma na linaloweza kufanya vitendo vya kinyama huku kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis akisema anawaombea wasichana hao kurejea makwao salama.
Mwandishi.Caro Robi/afp/dpa
Mhariri: Daniel Gakuba
DW SWAHILI

Posted by Editor on 17:31. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0

0 comments for NIGERIA: Juhudi za kimataifa zaongezeka kuwaokoa wasichana wa Nigeria

Post a Comment

Recent Entries

Recent Comments

Photo Gallery