MWALIMU WA RAIS KAGAME MSINGI BADO ASHIKA CHAKI
“UKIWA mwalimu, hakika wewe ni mtu muhimu sana katika malezi ya
mwanafunzi, kwani una nafasi kubwa ya kupenda mapema na kujifunza kutoka
kwako kwa sababu wewe ni mwalimu, mlezi na kioo cha mwanafunzi, haya
yakiunganishwa yanaweza kumtengeneza mwanafunzi bora,” anaandika Kahlil
Gibran katika kitabu chake, The Prophet `Mtume’, akioanisha majukumu
aliyonayo mwalimu.
Walimu kwa upande wao, wanasema zawadi kubwa kwao ni kuona wanafunzi
wao wanakuwa na mafanikio katika jamii. Na hicho ndicho kinachompa
furaha Augustin Nyabutsitsi, mwalimu mwenye umri wa miaka 74
aliyemfundisha Rais wa Rwanda, Paul Kagame katika madarasa ya sita na
saba kati ya mwaka 1967 na 1968. Nyabutsitsi ambaye bado ni mwalimu,
akifundisha katika Shule ya Le Bon Berger iliyopo Kimironko, Kigali,
anakiri kwamba alimwadhibu Kagame wakati anasoma Shule ya Msingi
Rwengoro iliyopo katika kambi ya wakimbizi Gahunge nchini Uganda.
Kwa mujibu wa mwandishi Marie-Anne Dushimana wa gazeti la Newtimes la
Rwanda, ikiwa imepita miaka 50 sasa, mwalimu huyo anasema anawakumbuka
vyema wanafunzi wake wa miaka hiyo. “Kagame alikuwa kama watoto wengine,
lakini alikuwa na utofauti, alikuwa mwerevu sana. Alipendelea masomo ya
Hisabati na Kiingereza. Alikuwa pia mdadisi, hakuacha kuuliza maswali
mpaka alipoona amejiridhisha,” anasema Nyabutsitsi na kuongeza kuwa,
daima Kagame alikuwa kinara darasani kwake.
Aidha, anakumbuka kuwa enzi hizo, Kagame alipendelea mno mchezo wa
soka, akitumia mpira wa `chandimu’ uliotengenezwa na kufungwa kwa kamba
za majani ya mgomba. Nyabutsitsi anasema hakuna kitu kinachofurahisha
kwa mwalimu, kama kuona mwanafunzi wake anamkumbuka na kutambua mchango
wa mwalimu katika maisha. Anasema kwa miaka mingi alikuwa na ndoto za
kuonana na mwanafunzi wake, Kagame, bila ya kujua kuwa Rais huyo wa sasa
wa Rwanda pia alikuwa na ndoto kama hizo.
Alisema hali hiyo siku alipokutana na Rais Kagame mkutanoni huko
Nyagatare, ambako aliuliza kama kuna yeyote anayefahamu anakoishi
mwalimu wake wa shule ya msingi, Augustin Nyabutsitsi. Alimkabidhi pia
jukumu hilo Profesa Manasseh Nshuti, akimtaka ahakikishe anamtafuta
Mwalimu Nyabutsitsi. Hatimaye, Kagame na mwalimu wake walikutana Januari
25, mwaka 2016.
Kwa sasa, Nyabutsitsi anaishi eneo la Kata ya Kinyinya katika wilaya
ya Gasabo katika kijiji cha kisasa maarufu kama “Kwa Dubai”. Anaishi
katika nyumba ya kisasa ya vyumba vinne aliyozawadiwa na Rais Kagame.
“Tulipokutana, sikuomba chochote kutoka kwake, lakini nilishangaa
alikuwa na taarifa nyingi juu yangu. Aliniambia amesikia naishi nyumba
ya kupanga, akaagiza nipatiwe nyumba ya kisasa. Hiki ndicho unachokiona
(anaonesha nyumba), ni zawadi ya Rais Kagame. Sikuwa na ndoto za
kumiliki nyumba ya aina hii.
Namshukuru sana,” alisema Nyabutsitsi huku sura yake ikiwa na
tabasamu pana. Anasema tukio hilo liliwashitua wengi, kiasi cha
kumiminika kuishuhudia. Dada wa Nyabutsitsi, Teddy Kawera (60) ambaye
pia ni Mwalimu katika shule ya Wellspring Academy ya jijini Kigali,
anasema kwa ujumla, zawadi hiyo ya nyumba ikiwa sawa na miujiza kwao.
“Tulikuwa tunaishi nyumba ya vyumba vitatu ya kupanga eneo la Kanombe
kwa gharama ya Faranga za Rwanda 150,000. Kodi ya nyumba sasa imebaki
historia, tunaishi kwa amani, bila ya kuumiza kichwa kufikiria kodi ya
pango, asante Rais Kagame,” anasema Kawera. Furaha ya Mwalimu Anasema
amekuwa mwenye furaha mno kuona baadhi ya wanafunzi wake wamekuwa watu
mashuhuri nchini Rwanda.
“Naamini nimekuwa na faida kwa nchi yangu. Kuna maofisa wengi wakubwa
na wanajeshi niliowafundisha, miongoni mwao ni Joseph Mugambage
anayefanya kazi na Rais Kagame, pia wamo Meja Rugira, Alexis Kagame na
wengine wengi. Orodha ni ndefu, lakini kinara wao ni Rais Kagame,”
anasema Nyabutsitsi. Akiwa katika fani ya ualimu kwa miaka 50 sasa,
Mwalimu Nyabutsitsi anasema siku zote amekuwa na wito wa kufundisha
watoto wa Rwanda. “Hakuna kinachonifurahisha kama kuona watu
niliowafundisha wanageuka kuwa muhimu katika nchini… ni bahati iliyoje,”
anasema.
Anasema mazingira ya kazi ya walimu, si kigezo cha kushindwa
kufundisha vyema, bali kiu ya kufanya kazi inapaswa kuwa mbele, ikiwa ni
pamoja na kuwa na upendo kwa wanafunzi. “Nashauri walimu wasiangalie
mazingira ya kazi tu, bali mwito kwanza. Wanafunzi wakiona wanapendwa,
hurudisha upendo kwa walimu wao na hata kuendeleza upendo kwa wengine.
Zawadi hii ya nyumba ni uthibitisho wa haya niyasemayo, nimefarijika
kukumbukwa na mwanafunzi wangu ambaye kwa sasa ni Rais wa Rwanda, Paul
Kagame,” anasema. Stevenson Mutunzi, mwalimu wa Shule ya Le Bon Berger,
anasema amepata fundisho kubwa kutoka kwa Mwalimu Nyabutsitsi. “Ametupa
fundisho kubwa la uvumilivu na kuipenda kazi licha ya changamoto kadhaa
zikiwemo za mishahara,” anasema.
Naye Egide Musoni, Mjumbe wa Kamati ya Wazazi wa shule ya Le Bon
Berger, anasema amefurahi kuona watoto wao wakifundishwa na mwalimu
aliyemfundisha pia mtu mashuhuri kama Rais Kagame. Baada ya kushuhudia
mabadiliko makubwa ambayo Rwanda imeyafikia kimaendeleo tangu mwaka
1994, anaamini miaka michache ijayo nchi hiyo chini ya Rais Kagame
itapiga hatua zaidi na zaidi, hivyo anamwombea maisha marefu
`mwanafunzi’ wake.
CHANZO HABARI LEO
Posted by Editor
on 14:24.
Filed under
eastafricannews,
feature,
gallery
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0