WAKUU WA SADC WAMPONGEZA RAIS MAGUFULI
WAKUU wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC), wamempongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri aliyoifanya
wakati akiwa mwenyekiti Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama
ya jumuiya hiyo.
Walitoa pongezi hizo jana wakati wakihitimisha Mkutano wao wa 37
mjini Pretoria, Afrika Kusini. Akizungumzia mambo muhimu yaliyojadiliwa
katika mkutano huo wa 37 wa SADC, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
ambaye alimwakilisha Rais Magufuli katika mkutano huo, alisema pamoja na
mambo mengine, SADC imetambua na kuthamini mchango wa Tanzania katika
kipindi cha uongozi wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama iliyokuwa chini
ya Rais Magufuli.
Alisema Tanzania imeshakuwa mwenyekiti wa asasi hiyo mara tatu kwa
nyakati tofauti, ambapo mara ya kwanza ilikuwa kipindi cha 2006/2007,
mara ya pili 2012/2013 na mara ya tatu kipindi cha Agosti 2016 hadi
Agosti 2017. Tanzania imemaliza kipindi chake cha Uenyekiti wa Asasi ya
SADC Agosti 19, 2017 wakati wa mkutano huo wa 37. Tanzania ilipokea
kijiti cha uongozi huo kutoka Msumbiji wakati wa Mkutano wa 36,
uliofanyika Swaziland Agosti 30, 2016.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana wakati wa Uenyekiti wa Tanzania
katika asasi hiyo ni kusimamia uchaguzi wa Bunge nchini Seychelles,
uliofanyika Septemba, 2016. Aidha katika kipindi hicho, Tanzania
ilisaidia kurejesha hali ya amani na utulivu nchini Lesotho, ambayo kwa
muda mrefu tangu 2014 imekuwa kwenye mgogoro wa kisiasa; pamoja na
kushughulikia matatizo ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC).
Wakati huo huo, Mkutano huo wa 37 wa SADC ulimuongezea muda mwingine
Mtanzania, Dk Stergomena Taxi kuendelea na wadhifa aliokuwa nao wa
Katibu Mtendaji wa SADC kwa kipindi cha miaka minne mingine, ambapo
atatumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2021. Dk Taxi alithibitishwa jana na
Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali na kuapishwa rasmi kushika
nafasi hiyo.
CHANZO HABARI LEO
Posted by Editor
on 14:01.
Filed under
eastafricannews,
feature,
gallery
.
You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0